Uwanja wa KMC Wafungiwa na TFF kwa Kukosa Vigezo



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia uwanja wa KMC uliopo Dar es Salaam kutumika kwa michezo ya Ligi, baada ya kubaini kuwa haukidhi vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.

Kwa mujibu wa TFF, miundombinu ya uwanja huo haijakidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa katika masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu, hali iliyopelekea kuchukuliwa kwa uamuzi huo.

Kutokana na hatua hiyo, klabu zote zinazoutumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia viwanja mbadala kwa mujibu wa Kanuni, hadi pale uwanja huo utakapofanyiwa marekebisho na kukaguliwa upya na TFF kabla ya kuruhusiwa kutumika tena.

TFF imesisitiza kuwa itaendelea kusimamia utekelezaji wa Kanuni na kuzitaka klabu zote nchini kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja ili kukidhi viwango vinavyotakiwa kwa michezo ya Ligi.