Waathirika wasimulia madhira nyumba zao 10 kuezuliwa Iringa

Iringa. Mvua kubwa zilizoambatana na upepo mkali zimeharibu nyumba 10 katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, hali iliyosababisha uharibifu wa mali, huku baadhi ya familia zikikosa makazi ya muda.

Wakizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo, Januari 29, 2026, Hezron Myengu, mmoja wa waathirika kutoka wilayani Mufindi, amesema kuwa upepo mkali uliezua paa la nyumba yake na kuharibu baadhi ya mali zake.

“Nilibaki na hofu wakati upepo mkali ukipiga paa la nyumba huku mvua ikinyesha kwa nguvu,” amesema Myengu.

Myengu ameongeza kuwa maji yaliingia ndani ya nyumba, vyombo vyote vilielea, na familia yake ilibaki nje bila makazi salama.

Naye Klensenzia Lumungo, mwathirika mwingine, amesema tukio lilitokea ghafla akiwa ndani ya nyumba pamoja na watoto wake, hali iliyomjaza hofu na kumfanya asije na cha kufanya.

Wakazi wengine wa Kata ya Mdabulo wamesema kuwa nyumba kumi zimeathirika, mabati yake yakipeperuka, na baadhi ya nyumba kuharibiwa sehemu za kulala na jikoni.

Wahanga hao wamesema walihitaji msaada wa haraka ili kurahisisha maisha yao na kuanza kurejea katika hali ya kawaida. Shirika la Rural Development Organization (RDO) limeanza kutoa msaada wa ukarabati wa nyumba zilizoharibiwa na kutoa mabati kwa wahanga.

Mkurugenzi wa RDO, Fidelise Filipatali, amesema kuwa baadhi ya nyumba zilianza kufanyiwa matengenezo mara moja kwa msaada wa vijana waliofunzwa katika vyuo vya ufundi, bila kusubiri msaada wa kutoka kwa wengine.

Diwani wa Kata ya Mdabulo, Marko Shayo, ameishukuru RDO kwa kuanza kusaidia kurejesha miundombinu iliyoharibiwa. Kwa bahati nzuri, mpaka sasa hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Exaud Kigahe amechangia mabati 100 kusaidia ukarabati wa nyumba zilizoharibiwa, jambo litakalo saidia kupunguza gharama kwa waathirika.

Ofisa Tarafa wa Ifwagi, Faraja Ndapo, amesema tathmini ya kina imefanyika na kubaini kuwa Kata ya Mdabulo ndiyo iliyoathirika zaidi, na mikakati ya kuhakikisha familia zote zinarejea katika makazi salama tayari imeanza.