Iringa. Wananchi wa mitaa ya Isakalilo na Kitwiru Manispaa ya Iringa wamesema changamoto ya ukosefu wa daraja la uhakika imeendelea kuwakwamisha kiuchumi na kijamii, wakidai kwamba ahadi za ujenzi wa daraja hilo na barabara ya lami zimekuwa zikitolewa kwa miaka mingi bila kutekelezwa.
Wakizungumza na Mwananchi leo Januari 29, 2026, wananchi hao wamesema changamoto ya ukosefu wa daraja la Isakalilo–Kitwiru umekuwa kikwazo kwa maendeleo yao na kwamba hali hiyo imeendelea kuwaathiri hasa msimu wa mvua.
Wananchi hao wamesema kuchelewa kwa utekelezaji wa mradi huo kumeendelea kuwanyima fursa za kunufaika na shughuli za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wakieleza kuwa mawasiliano duni yamekuwa yakisababisha wafanyabiashara na watalii kushindwa kufika kirahisi katika maeneo hayo.
“Daraja hili limekuwa ahadi ya muda mrefu, lakini hali halisi ni kwamba bado tunateseka hasa kipindi cha mvua,” amesema Agnes Chinya, mkazi wa Isakalilo ndani ya Manispaa ya Iringa.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Obedi Semba amesema wananchi wanaokaa kati ya Isakalilo na Kitwiru wanakumbwa na changamoto ya usafiri kutokana na umbali mrefu na uwepo wa daraja dogo lisilo salama linalokatiza Mto Ruaha.
“Daraja hilo ni la milingoti na ni hatarishi hasa kipindi cha mvua, jambo linalotuweka wakazi wa maeneo haya katika hatari tunapotaka kwenda au kurudi majumbani au kwenye shughuli zetu,” amesema Semba.
Semba amesema wafanyabiashara hulazimika kupita barabara ndefu zaidi ya Tosamaganga au Iringa Mjini – Ipogolo, hali inayoongeza gharama na kupunguza faida zao.
Kwa upande wake, Pius Kilyenyi, mkazi wa Kitwiru, amesema eneo hilo ni ukanda wenye maji mengi kutokana na uwepo wa Mto Ruaha, hali inayosababisha daraja hilo kufunikwa na maji mara kwa mara hasa kipindi cha mvua.
“Ukanda huu una maji sana, muda mwingine maji hujaa juu ya daraja na kufanya isiwezekane kabisa kuvuka, hali ambayo inatutesa sana wananchi,” amesema Kilyenyi.
Kwa upande wake, Manus Mawona, mkazi wa Isakalilo amebainisha kuwa wakati mwingine wananchi hulazimika kuvuka moja kwa moja ndani ya Mto Ruaha ili kupunguza umbali wa mitaa na kufika upande wa pili, hatua ambayo ni hatarishi hasa kwa watoto, wazee na wanawake.
“Watu wanapita mtoni kwa sababu hakuna njia mbadala ya karibu, lakini hii ni hatari kubwa sana,” amesema Mawona.
Kutokana na changamoto hiyo ya muda mrefu, Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Fadhili Ngajilo ameuliza swali bungeni, akihoji kuhusu hatma ya ujenzi wa daraja la Isakalilo – Kitwiru pamoja na kipande cha barabara ya lami chenye urefu wa kilomita tatu.
Ngajilo alisema daraja hilo limekuwa likiahidiwa kwa wananchi kwa zaidi ya miaka 20 bila utekelezaji, hali iliyosababisha kuendelea kudumaa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo husika.
Alisema kukamilika kwa mradi huo kungefungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi, hususani katika sekta ya utalii, kutokana na umuhimu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha katika uchumi wa Taifa.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Reuben Kagwila alisema daraja la Isakalilo–Kitwiru ni kiunganishi muhimu kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na limo chini ya Mradi wa Uendelezaji Miji Tanzania (TACTICS), awamu ya pili.
Naibu Waziri Kagwila alisema Serikali ipo katika hatua za usanifu wa mradi huo na mara baada ya kukamilika, utekelezaji utaanza rasmi, ukihusisha ujenzi wa daraja pamoja na barabara zenye urefu wa kilomita tatu.
Naibu Waziri Kagwila aliongeza kuwa Serikali imetenga Sh20 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ndani ya Manispaa ya Iringa, hatua inayotarajiwa kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kuboresha mawasiliano na kukuza utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.