WANANCHI KUNUFAIKA NA MRADI WA RAMANI ZETU, SAUTI ZETU

Na Mwandishi wetu, Morogoro.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imezindua mradi wezeshi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu”, unaolenga kuwajengea uwezo Wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani katika kukabiliana na Majanga.

Akizungumza katika Uzinduzi huo uliofanyika leo tarehe 29 Januari, 2026 Mkoani Morogoro Mkurugenzi Msaidizi wa Operesheni na Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu) Kanali Selestine Masalamado amesema, mradi huo umekuja wakati mufaka ambao jitihada kubwa zikiwa zinaendelea za kuzuia majanga ya asili maeneo mbalimbali ya nchi.

Aidha, ameeleza kuwa “tunahitaji uwepo wa data sahihi za wakati bila kusahau ushirikishwaji wa moja kwa moja wa jamii katika kuendelea kukabiliana na majanga ya asili na athari zake”.

“Mpango huu unaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayolenga kujenga Taifa lenye jamii imara yenye uwezo wa kutumia maarifa ya teknolojia katika kufanya maamuzi ya maendeleo” ameongeza Kanali Masalamado.

Naye, Mkurugenzi wa Taasisi ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ) Bw. Innocent Maholi, amesema Mradi huo unalenga kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, ikiwa ni pamoja maandalizi na usimamizi wa maafa kwa kutumia teknolojia na ushiriki wa wananchi katika ukusanyaji wa taarifa muhimu za maeneo yao.

“Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi na hatua za usimamizi madhubuti wa maafa ambazo sehemu muhimu ya safari ya kuelekea maendeleo endelevu na uchumi imara wa wananchi,” amebainisha.