ALIYEKUWA beki wa TRA United, Yassin Mustafa ameanza mazoezi na Coastal Union baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja akiwa mchezaji huru.
Beki huyo amerudi Coastal Union kwani tayari alishawahi kupita hapo miaka ya nyuma lakini pia amecheza Polisi Tanzania, Stand United, Mwadui United, Mtibwa Sugar na Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mustafa alisema: “Nimefika huku juzi, naendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiweka fiti na mechi zilizo mbele yetu, naamini kila kitu kitaenda vizuri kwa kuhakikisha naipambania timu kufikia malengo ya kuendelea kucheza ligi msimu ujao.
“Nimeaminiwa, hivyo nimepewa mkataba wa mwaka mmoja, sasa ni wakati wangu kuonyesha ni kwanini nimeipata nafasi hii, nitapambana kwa kusaidiana na wenzangu ili kuisogeza timu hii hatua moja hadi nyingine, hili linawezekana.”
Alisema anawaheshimu wachezaji wote waliopo ndani ya kikosi hicho, hamuhofii mtu kwasababu anaamini katika kipaji na uwezo alionao ikiwa ni pamoja na uzoefu alionao katika Ligi Kuu.
Coastal Union inaendelea kuboresha kikosi hadi sasa baadhi ya wachezaji waliomalizana nao ni Shiza Kichuya kutoka JKT Tanzania, Luician Kilua, Abdulkarim Segeja na James Msuva.