ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 435 ZATOLEWA KWA WAKULIMA

:::::::

BENKI ya Kilimo Tanzania (TADB) imetoa zaidi ya shilingi bilioni 435 kama mikopo kwa wakulima nchini, hatua iliyochochea maendeleo ya sekta ya kilimo na uzalishaji.

Mikopo hiyo imewezesha kufadhili jumla ya miradi 250, ikiwahusisha wakulima zaidi ya 203,000 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kuhusu mwenendo wa benki hiyo kwa kipindi cha mwaka 2025, Mkurugenzi wa Fedha wa TADB, Dkt. Kaanaeli Nnko, alisema mikopo hiyo imelenga kwa kiasi kikubwa wakulima wadogo na wa kati.


Alisema asilimia 67 ya mikopo hiyo imeelekezwa kwenye biashara za kilimo zenye thamani ya shilingi bilioni 429, hatua iliyoongeza tija na ushindani katika sekta hiyo.

Dkt. Nnko aliongeza kuwa benki hiyo pia imechangia kuinua uzalishaji wa viwanda pamoja na ujenzi wa maghala 44 ya kuhifadhi mazao, lengo likiwa ni kupunguza upotevu baada ya mavuno.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nnko alisema kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi 2025, benki hiyo imeongeza faida kwa asilimia 43.

Alieleza kuwa mali za benki zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 900 hadi kufikia shilingi trilioni 1.3, sambamba na kudhibiti kiwango cha mikopo chechefu hadi kufikia asilimia 2.5.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa TADB, Afia Sigge, alisema benki hiyo imepiga hatua katika maeneo mengine muhimu ya maendeleo ya wakulima.

Alitaja maeneo hayo kuwa ni utoaji wa elimu ya kifedha, uboreshaji wa riba, uwezeshaji wa sekta ya viwanda pamoja na mifuko ya dhamana kwa wakulima.

Sigge aliongeza kuwa benki imewekeza pia katika udhibiti wa upotevu wa mazao yakiwa shambani, hatua inayolenga kuongeza kipato cha wakulima na usalama wa chakula.