Unguja. Taasisi ya Aga Khan Foundation imezindua Mradi wa Maendeleo Plus unaohusisha mpango wa kilimo cha kuzalisha upya na lishe, unaolenga kuimarisha ustawi na uhuru wa wakulima kwa kuongeza mavuno na mapato kwa gharama ndogo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo uliofanyika jana Alhamisi Januari 29, 2025, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Aga Khan Foundation Tanzania, Atteeya Sumar amesema kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Afrika, kaya nyingi Zanzibar hutegemea zaidi masoko kuliko uzalishaji wa chakula nyumbani.
Amesema hali hiyo inachangia kuendelea kwa changamoto za lishe, hususan kwa wanawake na watoto.
Sumar amesema upungufu wa chakula huathiri moja kwa moja mahudhurio ya wanafunzi na uwezo wao wa kujifunza shuleni.
“Katika mfuko wa Aga Khan, tunaamini kuwa mustakabali wa usalama wa chakula na ustahimilivu wa tabianchi lazima uanze mapema. Ndiyo maana Maendeleo Plus hapa Zanzibar inatekelezwa kupitia shule. Shule si mahali pa kujifunzia tu, bali pia ni sehemu ambako watoto hupata chakula, tabia hujengwa na ujuzi husambazwa kutoka darasani hadi nyumbani na mashambani,” amesema Sumar.
Amesema nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara, wanawake huzalisha takribani asilimia 70 ya chakula, lakini chini ya asilimia 15 pekee hupata mafunzo ya kilimo au huduma za ugani. Pia, amesema mabadiliko ya tabianchi yanasababisha upungufu wa mavuno kwa asilimia 30 katika baadhi ya maeneo, hali inayojitokeza kwa sasa na siyo katika siku zijazo.
Kwa mujibu wa Aga Khan Foundation, mpango wa maendeleo tayari umefikia wakulima 60,000 barani Afrika, ambao wameripoti ongezeko la mavuno hadi asilimia 300 katika mwaka wa kwanza, upungufu wa gharama za uzalishaji hadi asilimia 95, pamoja na kuboreshwa kwa afya na lishe kwa familia zao.
Amesema katika shule 93 za Tanzania Bara, bustani za jikoni za kilimo cha kuzalisha upya sasa zinatoa chakula kwa wanafunzi.
Katika shule moja mkoani Morogoro, mahudhurio yaliongezeka kutoka asilimia 40 hadi asilimia 80 mara baada ya chakula kupatikana shuleni, huku wanafunzi wakipeleka ujuzi huo nyumbani, wazazi wakianzisha bustani na jamii kwa jumla kupata usalama wa chakula.
Naibu Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Dk Salim Soud Hamedamesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeupokea mradi huo kwa sababu unahimiza kilimo kinachotunza mazingira kwa kuepuka matumizi ya kemikali na kutumia eneo dogo kuzalisha mazao kwa wingi.
“Mradi huu ni muhimu kwetu kwa kuwa unaunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha usalama wa chakula Zanzibar. Ardhi yetu ni ndogo, hivyo tunapaswa kutumia mbinu za kilimo zinazohifadhi mazingira bila viuatilifu huku ukiimarisha mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Amesema kupitia mradi huo, vijana 12 wamepatiwa mafunzo maalumu na watapita katika shule za wilaya sita za Zanzibar kuwafundisha wanafunzi, ambao baadaye watawasambazia ujuzi huo wazazi wao nyumbani na hatimaye jamii zinazowazunguka.
Msimamizi wa Miradi ya Mazingira na Kilimo wa Aga Khan Foundation, Japhet Wangwe amesema mradi huo wa kilimo hai na lishe unalenga kulinda mazingira, ikolojia na viumbe hai.
“Kilimo kinachotawala kwa sasa kinategemea sana viuatilifu vya kikemikali, lakini kupitia mradi huu tunafundisha wakulima kutumia viuatilifu vya asili vinavyopatikana katika mazingira yao, ili kulinda udongo, kuboresha afya zetu na kulinda ustawi wa vizazi vijavyo,” amesema Wangwe.
Ameongeza kuwa,mbali na kuhifadhi mazingira, kilimo hicho ni rahisi na cha gharama nafuu kwa kuwa mbolea na dawa zinazotumika hutokana na mchanganyiko wa rasilimali za asili zinazopatikana katika jamii husika.
Mkurugenzi wa Kilimo na Umwagiliaji Zanzibar, Mussa Juma Abdulla amesema mradi huo ni muhimu kutokana na changamoto ya lishe inayolikabili Taifa hilo.
Amebainisha kuwa, Zanzibar tayari imezindua mpango mkakati wa kuendeleza kilimo mwaka jana, huku takwimu za lishe za mwaka 2022 zikionesha hali ya lishe kuwa katika kiwango cha asilimia 13 hadi 49.
“Kuendeleza programu kama hizi kutasaidia kwa kiasi kikubwa, lakini ingependeza zaidi kama zingefikia Zanzibar nzima badala ya wilaya sita pekee,” amesema.
Amesema endapo utekelezaji utafikia angalau asilimia 80, utasaidia kuboresha lishe shuleni ambako kwa sasa baadhi ya wanafunzi hupatiwa vyakula visivyo na lishe bora, hali itakayochangia kuboresha umakini na ufaulu wa masomo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Lady Fatemah Trust, Mukhtar Karim amesema katika hatua za awali, mradi huo utazifikia kaya 4,000 na wanufaika 15,000.
Amesema kupitia mradi huo, wakulima watapatiwa elimu ya kilimo chenye tija kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuzalisha chakula chenye lishe bora, kupunguza magonjwa na kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni, huku kinamama wakihakikishiwa upatikanaji wa chakula cha kutosha katika familia zao.