Barker atoa kauli nzito Simba ikiisaka rekodi ngumu CAF

BAADA ya kumalizana na Mashujaa katika mechi ya Ligi Kuu Bara, wekundu wa Msimbazi, Simba wamehamishia hesabu zao Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni mechi muhimu kushinda na ya uamuzi dhidi ya Esperance Sportive de Tunis itakayopigwa Jumapili wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam, huku kocha wa kikosi hicho akiwa hana maneno mengi, amesema: “Tulieni muone.”

Kwa nini mechi hii ni muhimu na yenye maamuzi? Hilo linatokana na kubeba mwelekeo wa timu hiyo kutinga robo fainali kufuatia kuanza vibaya katika mechi tatu za kwanza, ikiwa ni rekodi mbovu zaidi kwa Mnyama kwani tangu 2003 haijawahi kupoteza mechi tatu za kwanza mfululizo hatua ya makundi.

Katika mechi hiyo, Simba itakuwa ikitafuta pointi tatu za kwanza ambazo zitafanya kufufua matumaini ya kuisaka rekodi ya kibabe kwani tangu 2003 hakuna timu ambayo ilipoteza mechi tatu za kwanza halafu ikatinga hatua hiyo, kimahesabu, Simba inahitaji pointi tisa zilizosalia ili kutinga hatua hiyo bila ya kutegenea matokeo ya wapinzani wake.

Historia inaonyesha timu nyingi ambazo zilipoteza mechi tatu za kwanza zilimaliza hatua hiyo zikiburuza mkia au kushika nafasi ya tatu.

Msimu wa 2022–23, miamba ya soka la Cameroon, Coton Sport ilikumbana na hili ambalo Simba imekutana nalo kwa kuchapwa mechi zake tatu za kwanza katika hatua ya makundi.

Coton Sport ambayo ilikuwa kundi B ilianza kwa kuchapwa ugenini dhidi ya Al Ahly kwa mabao 3-0, iliporejea nyumbani katika mechi iliyofuata ilikumbana na kipigo kingine cha mabao 3-1 dhidi ya Mamelodi Sundowns, wakati wakiamini kuwa huenda watazindukia kwa Al Hilal ilikuwa ni mechi nyingine ambayo walikuwa nyumbani, walichapwa kwa mabao 2-1.


Shughuli ilikuwa pevu walichapwa tena katika mechi tatu ambazo zilisalia na kumaliza hatua ya makundi bila ya pointi wakati Mamelodi Sundowns na Al Ahly zikitinga robo fainali.

Mwaka 2017, AS Vita ilichapwa mechi zote sita za kundi D ikiwa imepangwa na Wydad Casablanca ya Morocco, Zanaco ya Zambia na Al Ahly ya Misri.

Ndani ya msimu huo, AS Vita ya DR Congo ikiwa kundi C nayo ilichapwa katika mechi zake tatu za kwanza dhidi ya Esperance de Tunis (ugenini) na Mamelodi Sundowns (nyumbani) zote kwa kipigo cha mabao 3-1 kwa kila mechi huku mechi yao ya tatu wakifungwa bao 1-0 dhidi ya Saint George.

Katika mechi tatu ambazo zilisalia, AS Vita ya DR Congo ikiwa na hesabu za kupindua meza, ililipa kisasi ikiwa nyumbani kwa kuichapa Saint George kwa mabao 2-1, wakaikaribisha Espérance de Tunis na kutoka nao sare ya mabao 2-2.

Hesabu zao zilifia Afrika Kusini ambako licha ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Mamelodi Sundowns, pointi tano ambazo walikusanya katika mechi hizo hazikutosha kutinga robo fainali na badala yake iliburuza mkia katika kundi hilo.

Msimu wa 2019–20, FC Platinum ikiwa kundi B ilichapwa mechi zake tatu za kwanza dhidi ya Al-Hilal (2-1), Étoile du Sahel (3-0) na Al-Ahly (2-0), ilishindwa kutoboa katika mechi zilizosalia iliambulia pointi moja tu na kuburuza mkia.

Mwaka 2015, MC El Eulma ya Algeria nayo iliburuza mkia katika msimamo wa kundi B ambalo lilikuwa na USM Alger, Al-Merrikh na ES Sétif baada ya kuchapwa katika mechi tatu za kwanza, ilimaliza hatua hiyo ikiwa na pointi moja tu.

“Ni kweli kwamba tumekutana na changamoto katika mechi zetu tatu za kwanza katika mashindano haya ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini huo sio mwisho wa safari yetu, bado tuna nafasi ya kufanya kitu katika mechi ambazo zimesalia. Tulieni muone,” amesema na kuongeza;


“Mechi dhidi ya Esperance ni muhimu sana kwetu, sio tu kwa sababu ya pointi, bali pia kwa morali ya kikosi chetu. Tunahitaji kuonyesha msimamo wetu kama timu. Tukipata matokeo chanya, inaweza kuwa mwanzo wa kurekebisha kilichotokea. Hii ni mechi ambayo tunahitaji sana, sapoti ya mashabiki wetu.”

Msimamo wa kundi D, unaongozwa na Stade Malien ya Mali yenye pointi saba, Esperance Tunis inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tano kisha Petro Atletico yenye pointi nne.

Hadi sasa, Simba ndio timu pekee katika hatua hii ambayo haijavuna pointi katika msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ilianza kwa kufungwa 1-0 nyumbani dhidi ya Petro Atletico, ikaenda ugenini kufungwa 2-1 na Stade Malien kisha 1-0 na Esperance.