Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka wazi mpango wake wa kuuza sehemu ya dhahabu iliyohifadhi kulingana na viashiria vya soko litakavyokuwa huku ikikanusha za mitandaoni kuwa fedha zitakazopatikana kupitia mauzo hayo zitaelekezwa katika uboreshaji wa miundombinu.
Haya yanasemwa ikiwa ni siku chache tangu kuchapishwa kwa taarifa katika mitandao ya kimataifa ikieleza mpango uliopo wa kuuza dhahabu hiyo kwa ajili kufadhili utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Januari 30, 2026, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Emmanuel Akaro amesema dhahabu hiyo inauzwa ili kuweka mizania sawa ikilinganishwa na ukomo waliokuwa wamejiwekea awali.
Amesema BoT ilikuwa imeweka ukomo wa Dola 2 bilioni za Marekani kama manunuzi ya dhahabu yatakayofanyika kabla ya kuongeza kufikia Dola 3 bilioni za Marekani.
“Tuliweka hii Dola 2 bilioni za Marekani baada ya kufanya uchambuzi wa vihatarishi na tuliona hii ilikuwa inafaa na sasa tumeweka ukomo wa Dola 3 bilioni ya Marekani na kile kinachozidi tunaona kabisa ni muda muafaka wa kukiuza ili tupate faida kwa sababu pia tunaendelea kununua dhahabu,” amesema.
Akaro ameongeza kuwa: “Wakati tunaanza mpango huu tulikuwa na ukomo wa Dola 350 milioni za Marekani, baadaye waliongeza hadi Dola 700 milioni za Marekani wakati ambao bei ya dhahabu inapanda jambo lililowafanya waweke ukomo wa Dola 2 bilioni za Marekani na sasa wako Dola 3 bilioni za Marekani.”
Amesema hadi jana Januari 29, 2026 BoT ilikuwa na dhahabu fedha yenye thamani ya Dola 1.18 bilioni za Marekani ambayo ikijumlishwa na dhahabu ambayo imesafishwa lakini haijafikia kiwango cha kuwa dhahabu fedha kimefikia Dola 3.24 bilioni za Marekani.
“Kwa jumla benki kuu ina dhahabu yenye thamani ya Dola za Marekani 3.24 ambayo ni sawa na tani 18.9 hadi jana Januari 29 ikiwa ni baada ya kuanza zoezi hilo Oktoba mosi mwaka 2024,” amesema.
Dhahabu iliyopo ni sawa na asilimia 36 ya mali za Tanzania zilizopo nje ya nchi.
Amesema kwa kawaida kitu chochote kinachoweza kupanda bei pia kinaweza kushuka huku akiweka bayana kuwa hali hiyo inafanya wachukue tahadhari hasa wanapoona dhahabu iliyopo imezidi kiwango kinachotakiwa inabidi wapunguze ili kuweka usawa.
“Mpango wa kuuza upo, tunauza lini inategemeana na soko likoje, kama sasa dhahabu imepanda bei sana ndani ya muda mfupi,” amesema Akaro.
Amesema kwa mfano, “ leo BoT ikiamua kuuza dhahabu fedha iliyonayo yenye zaidi ya thamani ya Dola za Marekani yenye thamani ya 3.188 bilioni inaweza kuipa Tanzania zaidi ya Sh7.14 trilioni kwa bei ya Januari 29 mwaka jana.
“Lakini dhahabu fedha hii tumenunua kwa Sh5.24 trilioni hivyo tukisema tuuze tutapata faida ya zaidi ya Sh1.6 trilioni lakini si kuda muafaka wa kuuza kidogo na kupata hiyo faida ndiyo swali linakuja hapo kuangalia vihatarishi kwani ikishuka na yenyewe ikishuka.”
Amesema kuuzwa kwa dhahabu hiyo hakutokani na msukumo wowote kutoka serikalini kwa kuwa, BoT iko huru katika kufanya shughuli zake ikiwamo kuamua namna inavyoweza kuwekeza katika fedha zipi za kigeni na kiasi gani huamuliwa na bodi.
Amesema BoT iko kwa ajili ya kuisaidia Serikali, kwani wanapowekeza huangalia sehemu salama ambazo haziwezi kuikwamisha kutoa msaada pindi unapohitajika.
“Ukiwekeza sehemu ambayo si salama, Serikali inataka kufanya malipo nje, tunataka kusaidia soko, nchi inataka kutumia fedha za kigeni na wewe umewekeza sehemu ambayo si salama ni hatari kwa usalama wa nchi ndiyo maana tunaweka sehemu yenye vihatarishi vidogo sana ili pale panapohitajika tuweze kuzitoa,” amesema.
Amesema baada ya mauzo kufanyika fedha hizo huwekezwa kwenye sarafu za kigeni ikiwamo Dola za Marekani na hawatauza kwa bei ya hasara kwani mara zote huuza kwa bei ya soko huku wakiangalia zaidi soko la Ulaya.
“Tunauza kupata thamani, kama thamani ya wakia moja ni Dola za Marekani 5,590 tukiuza tunataka kupata Dola 5,590 za Marekani,” amesema.
Amesema kwa sababu BoT imeendelea kununua dhahabu kila siku walifikia uamuzi wa kuuza dhahabu zilizonunuliwa siku za nyuma ili iweze kupata faida ambayo wanaamini Serikali nayo itanufaika.
Amesema wanaendelea kununua dhahabu kwa sababu wanataka kuongeza fedha za kigeni ili kuongeza kile kilichopo nchini.
Pia, ununuzi huo ni kuunga mkono soko la dhahabu hapa nchini sambamba kuongeza ufanyaji kazi wa kampuni zinazofanya uongezaji thamani.
Kwa mujibu wa soko la dunia, wakia moja ya dhahabu katika kipindi cha Januari mosi hadi 28 mwaka huu ilikiwa kati ya Dola 5,500 za Marekani kutoka Dola 4,300 za Marekani sawa na ongezeko la asilimia 26.
Kiwango hicho cha bei ikilinganishwa na ile iliyokuwapo mwaka jana imepanda kwa asilimia 60.
Akizungumzia akiba ya fedha za kigeni iliyopo amesema ni Dola 6.52 bilioni za Marekani ambazo zimewekwa katika fedha mbalimbali za kigeni ikiwamo Dola 3.84 bilioni za Marekani ambayo ni sawa na asilimia 59 ya akiba zote za fedha za kigeni.
Nyingine ni dhahabu thamani ya Dola 1.28 bilioni za Marekani huku Fedha ya China (Yuan) ndiyo inafuata ikiwa na usawa wa Dola 735 milioni ambayo ni sawa na asilimia 11 ya fedha zote za kigeni.