Burkina Faso yafuta vyama vyote vya siasa

Ouagadougou. Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imefanya uamuzi wa kihistoria kufuta rasmi vyama vyote vya siasa nchini humo, hatua iliyothibitishwa na baraza la mawaziri jana Januari 29, 2026.

Uamuzi huo unakuja ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za serikali ya kijeshi kudhibiti upinzani huku ikiendelea kukabiliana na vitisho vya usalama vinavyotokana na makundi yenye uhusiano na al-Qaeda na ISIL.

 Jana Alhamis, Januari 29, 2026 Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Emile Zerbo alisema serikali ilieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kujenga upya taifa, ikisisitiza kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ulikuwa umechangia migawanyiko mikubwa na kudhoofisha mshikamano wa kijamii.

Zerbo alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuimarisha utawala na sera za kitaifa.

Serikali pia imeamuru mali zote za vyama vya siasa vilivyofutwa kuhamishwa kwenye utunzaji wa serikali, huku ikipanga kutengeneza sheria mpya za kusimamia muundo wa vyama vya kisiasa utakaotungwa baadaye.

Kabla ya mapinduzi ya kijeshi mwaka 2022, Burkina Faso ilishuhudia ukuaji wa karibu vyama 100 vilivyorekebishwa kisheria, huku 15 vikishika viti bungeni baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Serikali ya kijeshi, inayosimamiwa na Kapteni Ibrahim Traoré, ilichukua madaraka kupitia mapinduzi ya Septemba 2022, miezi minane baada ya mapinduzi mengine kumuangusha rais aliyechaguliwa kidemokrasia, Roch Marc Kabore.

Katika kipindi cha uongozi wake, serikali imevunja mahusiano ya karibu na Ufaransa na badala yake kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na Russia ili kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi.

Aidha, serikali hiyo imetoa maagizo ya kusitisha upatikanaji wa tovuti za vyombo vya habari vya kimataifa kama BBC, Voice of America na Human Rights Watch mwaka 2024, hatua iliyokuwa ikichukuliwa kama sehemu ya kupiga marufuku upinzani na maoni yanayopingana na sera za serikali.

Burkina Faso pia imeungana na majirani zake Mali na Niger kuunda Muungano wa Nchi za Sahel (AES), mradi wa kiuchumi na kijeshi unaolenga kuimarisha ushirikiano baina ya serikali zinazokabiliwa na changamoto za kiusalama.

Habari hii imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa mashirika