CCM MOROGORO KUADHIMISHA MIAKA 49 KWA KUKAGUA ILANI NA MIRADI YA MAENDELEO

FARIDA MANGUBE, MOROGORO 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro kinatarajia kuadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama hicho Januari 31, 2026, kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM pamoja na kutembelea miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mvomero.

Akizungumza na Michuzi Tv Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro Nuru Ngereja, amesema maadhimisho ya sherehe hizo zitafanyika Turiani Wilani Mvomero na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joseph Masunga huku kilele  kitafanyika Februari 5 Halmashari ya Mlimba na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Mohamed Ali Kawaida.

Ngereja amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuhakikisha chama kinajitathmini kwa vitendo utekelezaji wa Ilani yake na kujionea maendeleo yanayotekelezwa kwa manufaa ya wananchi, badala ya kufanya sherehe za kawaida.

Ameeleza kuwa miongoni mwa miradi itakayokaguliwa ni Hospitali ya Wilaya ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, pamoja na miradi mingine ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya mkoa huo.

“Maadhimisho haya ni fursa ya chama kujipima, kuona utekelezaji wa Ilani na kusikiliza changamoto za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi,” amesema Ngereja.

Aidha, Katibu huyo wa Mkoa amezungumzia siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa zimeanza kuleta matokeo chanya ndani ya Mkoa wa Morogoro, hususani katika sekta ya afya kupitia utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.

Amesema mpango huo tayari umeanza kutekelezwa mkoani humo, ukiwa na lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila kikwazo cha gharama.

Ngereja ameongeza kuwa serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya mkoa huo, ikiwemo miradi ya maji, ujenzi na ukarabati wa barabara pamoja na ujenzi wa vituo vya afya, miradi ambayo inalenga kuboresha huduma za kijamii na kuinua maisha ya wananchi.

Amehitimisha kwa kusema CCM Mkoa wa Morogoro itaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi.