DED HALMASHAURI YA BUKOBA ATAJA MIRADI YA KIMKAKATI.

Na Diana Byera_Bukoba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Fatina Hussein Laay, ametaja miradi ya kimkakati itakayotekelezwa na Halmashauri katika mwaka wa fedha 2025/2026 mbele ya Baraza la Madiwani katika robo ya pili ya Halmashauri hiyo kwa lengo la kuitambulisha na kuijadili katika Baraza la Madiwani.

Fatina ameeleza hayo mbele ya Baraza kuwa Halmashauri iliibua miradi ya kimkakati kwa ajili ya uwekezaji kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, kuongeza fursa za ajira, kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuongeza chachu ya ukuaji wa miji katika maeneo ya vijiji yanayochipukia kimaendeleo.

Miradi hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.6 ni ujenzi wa ghala la dagaa na ununuzi wa mashine ya kukaushia dagaa Igabilo, ujenzi wa soko la ndizi Kemondo, uendelezaji wa stendi ya Kemondo na ujenzi wa jengo la kitega uchumi Shablidin.

Madiwani wa Halmashauri hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Sadoth Ijunga, wamepongeza utendaji wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na wakiahidi ushirikiano na usimamizi mkubwa wa mapato ya ndani ili kuongeza miradi inayogusa jamii itakayotekelezwa kwa fedha zitokanazo na mapato ya ndani.