………..
Na Sixmund Begashe, Arusha
Raisi wa Baraza la Usimamizi wa Mkataba wa Lusala, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, amewaagiza watendaji wa Mkataba wa Lusaka (LATF) kuhakikisha idadi ya wanachama inaongezeka wakati wa kipindi cha uongozi wake ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya ujangili na biashara haramu ya Wanyamapori na Misitu.
Dkt. Kijaji ameyasema hayo alipokutana na Sekretarieti ya Baraza hilo – Lusaka Agreement Task Force (LATF), jijini Arusha, kwa lengo la kupata uelewa wa pamoja wa utekelezaji wa kazi za Baraza hilo lenye dhamana kubwa ya ulinzi wa urithi wa maliasili.
Dkt. Kijaji amesema kuwa, ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye mhifadhi namba moja, ya kuhakikisha urithi wa Maliasili unalindwa vyema, hivyo atalinda dhamira hiyo kwa kutoa ushirikiano kwa sekretarieti hiyo ili kufikia malengo ya Baraza hilo.
Naye Mkurugenzi wa LATF Bw. Edward Phiri ameupongeza uongozi wa Serikali ya Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mkubwa kwa Baraza hilo hali inayochangia kutimiza majukumu yake vyema.
Baraza hilo, limeundwa na nchi zilizoungana katika kupambana na ujangali pamoja na biashara haramu za Wanyamapori na Misitu zinazovuka mipaka, Mkataba wake ulianzishwa mwaka 1994 huku Tanzania ikijiunga rasmi mwaka 1999 ambapo hadi sasa linanchi wananchama sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Zambia, Congo Brazzaville, Lesotho na Liberia.



