Dodoma. Serikali imesema itachukua hatua za kuzielekeza halmashauri zote nchini kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya ngozi kwa watu wenye ualbino, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera na miongozo ya utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Ijumaa, Januari 30, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Dk Jafar Seif wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM) Stella Ikupa, aliyehoji hatua zinazochukuliwa dhidi ya halmashauri zinazoshindwa kutenga fedha kwa ajili ya kununua mafuta ya wenye ualbino.
Akijibu swali hilo, Dk Seif amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilitenga Sh8.74 bilioni kwa ajili ya huduma za ustawi wa jamii, kati ya fedha hizo, Sh1.4 bilioni zilitengwa mahsusi kwa ununuzi wa mafuta ya ngozi kwa watu wenye ualbino.
Hata hivyo, amesema Serikali imeendelea kutoa maelekezo kwa halmashauri zote kuhakikisha zinazingatia wajibu wao wa kutenga fedha hizo na katika mwaka wa fedha 2025/26, jumla ya Sh1.9 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo.
“Katika fedha hizo, Sh182 milioni zimetengwa moja kwa moja kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye ualbino, wanufaika 14,655 wanatarajiwa kunufaika na huduma hiyo,” amesema Dk Seif.
Katika swali la nyongeza, Ikupa amehoji kiasi cha fedha kinachokwenda kwa kila mnufaika na kwa kila aina ya huduma, huku mbunge wa viti maalumu (kundi la watu wenye ulemavu) Mkoa wa Tabora (CCM), Nyamizi Mhoja akiuliza mpango wa Serikali wa kuajiri madaktari bingwa wa ngozi kwa ajili ya kuwahudumia wenye ualbino.
Akijibu maswali hayo ya nyongeza, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Ummy Nderiananga amesema Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya ngozi na kwamba ndani ya wiki mbili kuanzia sasa, kazi ya kuwasambazia walengwa itaanza rasmi.
Amesema Serikali pia itaendelea kusambaza vifaa maalumu vya kujikinga na mionzi ya jua (vitage) kwa wanafunzi wenye ualbino ili kuwawezesha kuhudhuria masomo yao katika mazingira salama.