Hii hapa jeuri ya Barker kwa Watunisia

USHINDI wa Simba juzi kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa umemshusha presha kocha wa kikosi hicho, Steven Barker, huku akiupongeza uongozi wa wekundu hao kwa kushusha vyuma vya maana katika kikosi hicho, kwani kitakwenda kuwasumbua Waarabu.

Simba jana iliifunga Mashujaa mabao 2-0, ikiwa ni ushindi baada ya kuchezea kichapo cha bao 1-0 kwenye mechi dhidi ya Esperance ya Tunisia, ikiwa ni hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker amesemaangalau matokeo waliyopata yametoa taswira ya maboresho ambayo wameendelea kuyafanya ili kuhakikisha timu hiyo inafanya vyema.


Amesemaangalau timu sasa imeanza kuonyesha hatua ya kuwa imara baada ya kufanya usajili, ambao umekwenda kuongeza kitu kikubwa na cha tofauti.

“Ushindi wa jana (juzi) umeshusha presha kwenye timu yetu na angalau wachezaji wameanza kuonyesha hatua ya kuwa imara baada ya nguvu iliyofanyika ya kuongeza mastaa kipindi hiki cha usajili.

“Usajili ulioufanyika utairudisha Simba ambayo mashabiki na viongozi wanaitaka na sasa hatua inayokwenda ni kuendelea kuwaunganisha wachezaji ili kuelewana, hasa wanapokuwa uwanjani kutokana na nafasi zao.”


Katika mechi dhidi ya Mashujaa, mfungaji wa mabao alikuwa Libasse Gueye dakika ya 28, mmoja kati ya wachezaji waliosajiliwa hivi karibuni, huku la pili likiwa ni penati iliyopigwa na Kibu Denis na kuzaa bao.

Barker amesemakikosi anachokiona sasa kinampa uhakika wa kufanya vyema kwenye mechi dhidi ya Waarabu wa Tunisia, kwani kina mabadiliko makubwa kulinganisha na walivyokutana awali.

Aliongeza, “Matokeo ya sasa ni morali nzuri kabla ya kwenda kucheza na Esperance, kwa kuwa Waarabu hao watakutana na Simba tofauti Jumapili.”


Simba itakutana na Esperance tena Jumapili, Februari Mosi, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo jijini Dar es Salaam saa 10:00 jioni.