Huu hapa uamuzi wa mahakama sakata la Mwambe kunyang’anywa pasipoti

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Saa imeridhia kumsikiliza waziri wa zamani, Geofrey Mwambe kuhusiana na sakata la kunyang’anywa pasipoti zake mbili, na za familia yake.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa, Januari 30, 2026 na Jaji David Ngunyale baada ya kukubaliana na maombi yake ya kibali cha kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kuomba amri ya kumlazimisha Kamishna Mkuu wa Uhamiaji kumrejeshea pasipoti zake hizo.

Hata hivyo, Mahakama hiyo imesema kuwa ruhusa inamhusu Mwambe peke yake na si mke na watoto, huku ikieleza kuwa, kuna utaratibu wa kisheria wa kufungua maombi kama hayo kwa niaba ya watu wengine, unaopaswa kufuatwa.

Mwambe ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mbunge wa Masasi, Mtwara (CCM), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Waziri wa Viwanda na Biashara amenyang’anywa na maofisa uhamiajhi pasipoti zake  wakiwa safarini na familia yake. 

Kwa mujibu wa kiapo chake kilichounga mkono hati ya maombi, Mwambe alieleza kuwa yeye ni Mtanzania na mmiliki wa hati ya kusafiria namba TDE011349 na mkewe Tumaini Jason Kyando anamiliki hati ya kusafiria namba TAE181501.

Pia, wana watoto wao watatu ambao bado ni wadogo, Kinkil Geoffrey Mwambe, anayemiliki hati ya kusafiria namba TAE923387; Karen-pracht Geoffrey Mwambe, mwenye hati namba TAE925212 na Kathrin-lena Geoffrey Mwambe, mwenye hati namba TAE903654.

Alidai kuwa, Desemba 17, 2025, alisafari kuelekea Ujerumani kwa ajili ya matibabu kupitia Kenya alipotoa pasipoti yake kugongewa mhuri katika Kituo cha Mpaka cha Namanga, ofisa uhamiaji Patrick Mkande aliichukua pasipoti yake hiyo na akakataa kumrudishia, hivyo akalazimika kurudi Dar es Salaam.

Pia, mke wake na watoto wao watatu siku hiyo walitarajiwa kusafiri kupitia Mpaka wa Sirari, Musoma Mara kwenda likizo ya Sikuku ya Krismasi katika Hifadhi ya Taifa ya Masai Mara  na baadaye kuungana naye Nairobi kwa ajili ya taratibu za kwenda Ujerumani kwa matibabu yake.

Hata hivyo, nao pasipoti zao zilikamatwa na maofisa wa uhamiaji, wakaamua kurudi Dar es Salaam.

Hivyo, kupitia mawakili wake Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu alifungua shauri mahakamani hapo dhidi ya Kamishna Mkuu wa Uhamiaji na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika shauri hilo alilolifungua chini ya hati ya dharura, Mwambe aliomba Mahakama hiyo imruhusu kufungua shauri la mapitio ya Mahakama ili imuamuru kamishna wa uhamiaji kuachia na kukabidhi pasipoti yake na ya mke na watoto wao.

Katika mashauri ya maombi ya kibali cha kufungua shauri la mapitio ya Mahakama, mwombaji ili apewe kibali hicho anapaswa kuionesha mahakama kuwa amekidhi vigezo vyote vitatu vilivyowekwa kisheria.

Vigezo hivyo ni kama mwombaji ameonesha kuwa, mosi kuna suala linalobishaniwa, pili, amefungua maombi hayo ndani ya muda uliowekwa kisheria yaani miezi sita tangu kutokea kwa suala linalobishaniwa na tatu, kuwa ana masilahi stahiki katika suala husika.

Wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Januari 26, 2026, hoja pekee iliyobishaniwa na ambayo ndio Mahakama imeitolea uamuzi ni kama mwombaji ana masilahi stahiki.

Jaji Ngunyale baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake alioutoa leo Ijumaa, Januari 30,2026, amekubalina na mawakili wa Mwambe kuwa ana masilahi stahiki katika suala analolilalamikia.

Pia, Jaji Ngunyale amekubaliana na hoja ya Wakili wa Serikali Mkuu, Vivian Method kuwa mwombaji hana mamlaka ya kuomba nafuu anazoziomba, katika shauri hilo kwa niaba ya watu wengine akikubalina naye pia kuwa, kuna utaratibu unaopaswa kuzingatiwa wa kuomba nafuu hizo kwa niaba ya watu wengine.

“Mahakama hii baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, imeanza kwa kujiuliza kama mleta maombi hawezi kuomba kwa niaba ya mke na watoto wake, je ni sahihi kutupilia mbali maombi yenyewe?,” amehoji Jaji Ngunyale na kujibu swali hilo kuwa hapana. 

“Hivyo inakubaliana na mwombaji kuwa ameweza kuonesha kuwa ana masilahi stahiki katika suala hilo na inatoa kibali kwa mwombaji mwenyewe  cha kufungua shauri la mapitio  ya Mahakama dhidi ya wajibu maombi, ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi huu,” amesema Jaji Ngunyale.

“Lakini kwa hao watu wengine waliotajwa kwenye maombi haya (mke na watoto), anaweza kutumia utaratibu mwingine wa kisheria.”

Akizungumzia uamuzi huo, Wakili wa Mwasipu amesema baada ya kupata kibali hicho kwa Mwambe, watafungua shauri hilo mapema la kuiomba Mahakama imrudishie pasipoti zake na kwamba kuhusu mkewe na watoto watatumia utaratibu mwingine wa kisheria kupambana kurejeshewa pasipoti zao.

Wakili Mpoki  akizungumzia hoja hiyo  ameieleza Mahakama kuwa mwombaji ana masilahi juu ya pasipoti zake na za familia yake ambazo zimeshikiliwa.

Amedai kwamba,masilahi yanatokana na ukweli kwamba mke wake ndiye mtu aliyetakiwa kumsindikiza kwenda kwenye matibabu.

‎Ameongeza kuwa, na watoto pia wana haki ya kuwa na pasipoti zao isipokuwa kama wamefanya makosa chini ya Sheria ya Uhamiaji au Sheria ya Pasipoti na Hati za Kusafiria Tanzania.

‎”Hakuna chochote ambacho Mwambe na familia yake wamefanya mpaka pasipoti zao zishikiliwe. Kwa hiyo masilahi ya mwombaji yanapatikana hapo na wamiliki hawajafanya jambo lolote la kufanya zishikiliwe,” amesema Wakili Mpoki.

“Sheria inataka kwamba, kwa sababu pasipoti hizo ni halali zinapaswa ziwe mikononi mwa wamiliki na Serikali haina masilahi ya kuwa nazo.‎ Kitendo cha kunyang’anywa ni ukiukwaji wa haki ya Kikatiba ya uhuru wa mtu kwenda atakako mtu.”

‎Akijibu hoja hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Wakili Method aliirejesha Mahakama katika kanuni ya 4 ya Kanuni za Marekebisho ya Sheria (Ajali Mbaya na Masharti Mengineyo) (Utaratibu wa Mapitio ya Kimahakama na Ada).

Amedai kuwa, kwa mujibu wa kanuni hiyo  ni mtu mwenye masilahi stahiki anayeweza kufungua maombi ya kibali cha mapitio ya Mahakama.

Amedai kuwa, Mwambe hana haki ya kisheria kufungua maombi kwa niaba ya hao anaowaita mkewe na watoto wake, kuiomba Mahakama imuamuru Kamishna Mkuu Uhamiaji kuwarejeshea pasipoti.

‎”Ni hoja yetu kwamba suala la pasipoti ni la mtu binafsi chini ya Sheria ya Pasipoti  na Nyaraka za Kusafiria Tanzania, Sura 42 Rekebu ya mwaka 2023 ambayo kifungu cha 2 inaeleza kuwa pasipoti inatolewa kwa mtu binafsi,” amesema Wakili Method.

‎”Katika maombi haya, hao anaowaita mkewe na watoto wake si waombaji katika hilo shauri. Hivyo, mwombaji peke yake hawezi kuwa na masilahi ya kuomba pasipoti kwa ajili ya anaosema ni mke na watoro wake .” 

Wakili Method amesisitiza kuwa ingawa Mwambe ameeleza katika kiapo chake kuwa amefungua maombi hayo kwa niaba ya watoto wake, lakini kuna utaratibu wa kufungua maombi kwa niaba ya watoto wadogo na kwamba haujafuatwa.

‎‎Amedai kuwa, ingawa mwombaji yeye binafsi (Mwambe) ana masilahi stahiki lakini kwa kuleta maombi pamoja na anaosema ni mkewe na watoto wake ambao hana haki kufungua maombi kwa niaba yao kunayafanya yasiwe sawasawa mbele ya Mahakama.

‎Hivyo, ameiomba Mahakama iyatupilie mbali maombi hayo kwa gharama.

‎Wakili Mpoki akijibu hoja hizo amedai kuwa katika mashauri ya mapitio ya Mahakama suala la haki ya kufungua shauri (locus standi) haitumiki, kwani hutumika katika mashauri ya madai ya kawaida na kwamba katika mashauri ya mapitio ya Mahakama mwombaji anapaswa kuonesha masilahi stahiki.

“Masilahi stahiki ni haki ya mtu kuzuiwa kusafiri na kuongozana na mtu wa kumsaidia, ndiyo tunayozungumzia. Kwa sababu hizo ana masilahi stahiki,” amesema wakili Mpoki na kuungwa mkono na Wakili Mwasipu kuwa kesi zilizorejewa na wajibu maombi hazifanani na shauri hilo.