Mapema tu leo Al Ahly imeonyesha kuanza kutishwa na hali ya joto kwenye Uwanja wa New Amaan Complex mjini Unguja ikisaka maji kwa haraka kabla ya kuanza kwa mazoezi.
Timu hiyo ambayo kesho itakuwa mgeni wa Yanga kwenye mchezo wa nne wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imetua Uwanja Amaan saa 9:55 tayari kwa mazoezi ya mwisho ambapo mara baada makocha kuzigusa nyasi wakaomba umwagiwe maji haraka.
Maofisa wa Al Ahly wameonekana wakiwahimiza wasimamizi wa Uwanja wa Amaan kufungulia mabomba haraka kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo.
Kocha Jesse Thorup ameonekana akiwarudisha wachezaji wake vyumbani akiwaambia joto ni kali uwanjani na wataitwa baada ya mabomba kufunguliwa.
Dakika chache baadaye baada ya mabomba hayo kufunguliwa timu hiyo ikaendelea na ratiba ya mazoezi kwenye uwanja huo.
Wakati Ahly ikianza mazoezi ikapishana na waamuzi wa mchezo huo kutoka Cameroon ambapo maofisa wa juu wa klabu hiyo wamesikika wakisisitiza kwamba dakika za mapumziko kunywa maji (water break) wakiomba yazingatiwe kutokana na hali ya joto.
Leo, hali ya hewa Zanzibar inasoma nyuzi joto 31 ambapo Al Ahly imeonyesha wasiwasi wa wachezaji kukabiliana nayo.