Kocha Alliance Girls asepa, timu yabariki

HATIMAYE baada ya tetesi za muda mrefu, Kocha Mkuu wa Alliance Girls, Sultan Juma ameondoka klabuni hapo na kwenda kutafuta changamoto kwingine baada ya mazungumzo ya kuongeza mkataba kushindwa kufanikiwa.

Juma ameondoka pamoja na wasaidizi wake, Amani Luambano na Masoud Bakari (kocha wa makipa), ambao walisaini mkataba wa mwaka mmoja msimu uliopita.

Chini ya benchi hilo la ufundi, Alliance ilimaliza ya tano msimu uliopita kwenye Ligi Kuu ya Wanawake na msimu huu tayari katika mechi 10 inashika nafasi ya nne nyuma ya Simba Queens, Yanga Princess na JKT Queens, ikikusanya alama 19 baada ya kushinda mechi sita, sare moja na kupoteza tatu.

Sultan Juma amedumu Alliance kwa takribani miaka 10 akiwa kocha msaidizi chini ya Ezekiel Chobanka, ambapo msimu uliopita aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu baada ya Chobanka kutimkia Ceassia Queens ya Iringa.

Akizungumza jijini hapa, Juma aliishukuru Alliance kwa kumpa ushirikiano na nafasi ya kuonyesha uwezo wake, lakini akasisitiza wakati umefika wa kutafuta changamoto kwingine.

”Nimefikia muafaka wa kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine, ninachosisitiza ni kwa wachezaji wa Alliance kuendelea kujituma ili watimize malengo ya timu,” amesemaJuma na kuongeza;

”Nawashukuru Alliance kwa muda wote ambao nimekaa hapa nimeitumikia taasisi hii kwa zaidi ya miaka 10, nawashukuru wote wanaohusika kwa kunipa ushirikiano nawashukuru wachezaji wangu pia.”

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Alliance Girls, klabu hiyo imempa baraka zote kocha huyo baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili kila mmoja kuanza safari mpya.

”Uongozi wa Alliance Girls tunatoa shukrani za dhati kwa Kocha Sultan Juma kwa mchango wake mkubwa ndani ya klabu yetu. Kazi, nidhamu na moyo wake wa kujituma vimeacha alama isiyofutika kwetu sote,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza;

”Kama viongozi, kwa makubaliano ya pamoja na kwa moyo mmoja, tumekubali  Kocha Sultan Juma kwenda kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine. Tunatambua na kuthamini kuwa Alliance Sports Academy ni nyumbani kwake  na milango itakuwa wazi muda wowote.”