Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imetangaza kusitisha huduma kwa kampuni nne za mifumo ya tiketi mtandao ambazo hazijaidhinishwa kisheria na kutoa muda kwa wamiliki wa mabasi waliokuwa wakitumia mifumo hiyo kujitoa na kujisajili kwenye mifumo iliyoidhinishwa rasmi.
Kampuni zilizositishwa kutoa huduma ni Tiketi rafiki, Safari yetu, Safiri tiketi na Exbite tiketi. Kutokana na hali hiyo, Latra ilitoa notisi ya mwisho ikielekeza kuwa mifumo yote isiyokidhi matakwa isimamishe huduma kuanzia Januari 14, 2026, na wamiliki wa mabasi kuhamia kwenye mifumo iliyoidhinishwa kabla ya Februari 15, 2026.
Uamuzi huo umetokana na utekelezaji wa Kanuni za Tiketi Mtandao za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini za mwaka 2024, zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 23 Januari 31, 2024.
Kanuni hizo zinaelekeza kuwa mfumo wowote wa tiketi mtandao unatakiwa kujaribiwa, kuidhinishwa na kupewa kibali na Latra kabla ya kutumika rasmi katika kutoa huduma kwa vyombo vya usafiri wa umma, ikiwamo mabasi ya safari za mikoani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Januari 30,2026 , Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Latra, Salum Pazzy amesema tangu kuanza kwa utekelezaji wa kanuni Oktoba 2024, Latra imefanya vikao zaidi ya saba na watoa huduma wa mifumo ya tiketi mtandao kwa lengo la kutoa elimu na kuwakumbusha masharti ya usajili.
Amesema katika vikao hivyo, ilikubaliwa hadi Juni 30, 2025, watoa huduma wote wawe wamekamilisha masharti ya usajili. Hata hivyo, kufikia Desemba 30, 2025, ni watoa huduma watano tu kati ya 15 waliokuwa sokoni waliokuwa wamekamilisha masharti yote lakini hadi kufikia Januari 30, 2026 ni watoa huduma 10 pekee walikuwa wamekidhi vigezo.
“Hatua hiyo inaendana na msisitizo wa Serikali wa kuhakikisha shughuli zote za kifedha zinafanyika kupitia mifumo ya kielektroniki,” amesema Pazzy.
Kwa mujibu wa Pazzy kifungu cha 5 cha kanuni hiyo, mfumo wa tiketi mtandao unatakiwa kutimiza vigezo ambavyo ni umiliki wake uwe wa taasisi ya Serikali, chama cha ushirika au kampuni iliyosajiliwa Tanzania.
Pia, uwe umeunganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Malipo ya Serikali (GePG) na uwezo wa kuunganishwa na mifumo ya Latra na mifumo mingine ya Serikali inapohitajika.
Vigezo vingine ni uwe umeidhinishwa na mamlaka husika, umiliki wake uwe wa Mtanzania na mmiliki awe na wataalamu wenye sifa kwenye fani husika na mifumo madhubuti ya ulinzi wa taarifa na kukabiliana na uhalifu wa kimtandao (cybercrime).
Amesema utekelezaji wa vigezo hivyo unalenga kuwasaidia watoa huduma kupata mapato kwa ufanisi bila kupitia watu wa kati, abiria kununua tiketi kwa uwazi bila ulanguzi na kuiwezesha Serikali kusimamia sekta ya usafiri kwa ufanisi zaidi na kuongeza mapato.
Akizungumza na Mwananchi Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustapha Mwalongo amesema siku zilizotolewa kwa wenye mabasi ni chache hivyo ingewekwa hata miezi miwili.
“Siku hizo zilizowekwa ni siku chache kwa sababu inahitajika elimu kwa watoa huduma wa mabasi kuelezwa kampuni zisizotambulika hususani kwa wale wa mikoani,” amesema Mwalongo.
Amesema wiki mbili ni siku chache kumfikia mtu aliyepo Katoro ili kuelimishwa, hivyo elimu ni jambo moja na uelewa ni jambo lingine hivyo Latra wangewasaidia kwa kuongeza siku ili wasiwapoteze watoa huduma wa mabasi.