Madhara yasababishwayo na ‘stress’ | Mwananchi

Mkazo au shinikizo kitabibu hujulikana kwa jina la ‘Stress’, ni hali ya mwitikio wa mwili kujihami au kujibu mapigo baada ya kupata tishio, changamoto, kuwa katika hatari au mahitaji ambayo mara nyingi husababishwa na wasiwasi unaomwelemea.

Shinikizo la jumla lina athari kimwili pale linapoathiri akili na hisia na ndipo hujulikana kama shinikizo la akili.

Hali hii husababisha mfumo wa neva kuamrisha utiririshwajI wa homoni zinazoleta mabadiliko mwilini.

Hali hii huwa na faida zake, kwani ndio inayotuepusha katika hatari ikitupa chaguzi mbili dhidi ya hatari ikiwamo kupambana au kukikimbia. Wakati mwingine mwili ukielemewa zaidi huleta hali ya kuzimia.

Inaweza kuwa ya kawaida ya muda mfupi na kusababisha ongezeko la muda la shinikizo la damu, hii ni kutokana na mwili kutiririsha homoni kama vile adrenaline na cortisol, ambazo huongeza kasi ya mapigo ya moyo.

Dalili za shinikizo huwa ni kukosa utulivu, hasira, huzuni, matatizo ya kulala, mkazo wa misuli, ugumu wa kuzingatia, maumivu ya kichwa, uchovu, mabadiliko ya kula na kujitenga.

Shinikizo la mwili lisipodhibitiwa na kudumu muda mrefu linaweza kusababisha kujitokeza kwa magonjwa kadhaa ikiwamo magonjwa ya moyo hasa shinikizo la damu na shambulizi la moyo. Vile vile kuweza kusababisha uharibifu wa mishipa midogo ya damu, moyo na figo.

Kwa ujumla, tafiti zinaonyesha kwamba shinikizo halisababishi shinikizo la juu la damu moja kwa moja, lakini linaweza kuchangia kujitokeza kwake hasa hali hiyo inapokuja mara kwa mara.

Tatizo hili linapodumu kwa muda mrefu linamweka mwathirika katika hatari pia ya kupata magonjwa ya akili, ukosefu wa hamu ya kujamiana, ugumba, kupata wazimu, kujiua, kujikataa na uharibifu wa ngozi.

Miaka ya nyuma shinikizo la juu la damu ilikuwa ikionekana zaidi kwa watu wenye unene uliokithiri zaidi wenye kipato kikubwa na maisha bora ya kifahari.

Lakini miaka ya sasa hata wale wenye uwezo mdogo na kutokuwa na kazi wamekuwa wakijikuta wakiwa na maradhi ya shinikizo la juu la damu, yaani msukumo ambao unazidi kile kiwango cha kawaida ambacho ni 120/80.

Miaka ya karibuni shinikizo limekuwa likichangia kwa wastani shinikizo la juu la damu na magonjwa mengine ikiwamo kiharusi, ugonjwa wa kusahau na shambulizi la moyo.

Mifarakano, ugumu wa maisha, kuchanganyikiwa, kufiwa, kutokua na ajira, kuumwa maradhi sugu na kukata tamaa ni moja ya mambo ya mambo yanayochangia shinikizo.

Wenye shinikizo huweza kuvamia tabia na mienendo isiyofaa ya kukabiliana na hali hiyo kama vile kula lishe duni, kutofanya mazoezi, uvutaji sigara na unywaji pombe kupita kiasi.

Haya yote huongeza hatari ya shinikizo la juu la damu.

Ili kudhibiti hali ya shinikizo, ni muhimu kujihusisha na shughuli za kila siku na kujiweka mbali na jambo linalokuletea shinikizo.

Badili mienendo na mitindo ya maisha ikiwamo kufanya mazoezi, ulaji mzuri, pumzika na lala usingizi angalau saa 8-10 kwa usiku mmoja.

Vile vile kujiburudisha kiakili, kupumua, kujitafakari na kuvuta hisia, mazoezi laini kama yoga au usingaji na kujichanganya na jamiii, fanya ibada, kazi za jamii au na matembezi ya pamoja.

Ni muhimu mwathirika kufika au kufikishwa mapema katika huduma za afya kabla ya madhara zaidi kutokea.