Dodoma. Kaburi la marehemu Peter Kanyamala (85), mkazi wa Mtaa wa Mbalawala jijini Dodoma limefukuliwa na watu wasiojulikana wiki mbili baada ya kuzikwa na uchunguzi wa mwili wake umebaini kuwa sehemu ya nyama ilikatwa chini ya titi la kushoto.
Marehemu Kanyamala alifariki dunia Januari 15, 2026, baada ya kugongwa na gari jijini Dar es Salaam, kisha mwili wake kusafirishwa na kuzikwa Januari 19, 2026, katika Mtaa wa Mbalawala, Dodoma.
Hata hivyo, jana Ijumaa Januari 29, 2026, kaburi lake lilikutwa limefukuliwa na watu wasiojulikana.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 30, 2026, mtoto wa marehemu, Samweli Kanyamala amesema baba yao alifariki dunia baada ya kugongwa na gari alipokuwa akivuka barabara jijini Dar es Salaam, akielekea kwenye shughuli zake Kariakoo.
Amesema familia ilipata taarifa za ajali hiyo kupitia askari wa usalama barabarani ambaye aliwajulisha kuwa marehemu alikuwa amelazwa Hospitali ya Mloganzila.
Hata hivyo, amesema walipofika hospitalini hapo waliambiwa baba yao tayari amefariki dunia.
“Baada ya hapo tulifanya vikao vya mazishi na kukubaliana kuwa tumzike baba nyumbani Dodoma. Tulisaidiwa na vikundi vyetu vya kusaidiana Dar es Salaam, tukamsafirisha na kumzika mzee wetu kwenye nyumba yake ya milele,” amesema Kanyamala.
Amesema jana familia ilipata taarifa ya kushtua kutoka kwa mwenyekiti wa Mtaa wa Mbalawala, aliyewajulisha kuwa, kaburi la baba yao limefukuliwa na watu wasiojulikana, huku askari polisi wakiwa tayari eneo la tukio wakihitaji maelezo kuhusu majeraha aliyokuwa nayo marehemu wakati wa ajali.
“Walimhoji kaka yangu ambaye aliukagua mwili wa mzee hospitalini. Tulishangazwa na jeraha la upande wa kushoto chini ya titi kwa kuwa halikuwepo awali. Taarifa hizo zimelazimu nifunge safari kuja Dodoma kujua kinachoendelea, ilhali hata uchungu wa kumpoteza mzee bado haujaisha,” amesema.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mbalawala, Obadia Shija amesema alipokea taarifa za tukio hilo jana saa 12 asubuhi, ndipo alipoenda eneo la tukio na kukuta kaburi hilo limefukuliwa, mfuniko wa jeneza ukiwa wazi na shati alilozikwa nalo marehemu likiwa limepandishwa kifuani.
Amesema aliwajulisha polisi ambao walifika wakiwa na daktari na kufanya uchunguzi wa mwili huo na ilibainika kuwa, kulikuwa na nyama iliyokatwa chini ya titi la kushoto la marehemu.
“Baada ya uchunguzi huo tuliruhusiwa kuuzika mwili upya. Hadi sasa sijapata taarifa ya mtu yeyote kukamatwa kuhusiana na tukio hili la aibu kwa mtaa wetu. Ndugu wengine wa marehemu wapo njiani kuja baada ya kuwajulisha,” amesema Shija.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera amekiri kaburi hilo kukutwa limefukuliwa jana saa 12 asubuhi na kwamba, uchunguzi unaendelea kubaini waliohusika na tukio hilo.
Ametoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya kufukua makaburi kiholela, akisema ni kinyume cha sheria ya uzikaji, na kwamba ufukuaji wa kaburi unapaswa kufanywa kwa kufuata taratibu ikiwamo kupata kibali cha Mahakama.
Amesema jeraha lililobainika chini ya titi la kushoto la marehemu ni tofauti na majeraha aliyoyapata kwenye ajali iliyosababisha kifo chake, hali inayoashiria kuwa waliofukua kaburi hilo waliondoka na kipande hicho cha nyama.
“Ufukuaji wa makaburi kiholela unasababisha taharuki kwa jamii, kumvunjia heshima marehemu na ni kinyume cha sheria za afya na usalama, kwani unaweza kusababisha madhara ya kiafya endapo utafanyika bila kufuata taratibu,” amesema Kamanda Hyera.