Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametangaza mpango kabambe wa kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa njia ya barabara utakaorahisisha usafiri, kuongeza ufanisi na kukuza pato la Taifa.
Mpango huo unaoitwa ‘Expressways Master Plan’ umeanza kutekelezwa na wataalamu wazalendo wa Tanzania kwa ushirikiano na wenzao kutoka Korea Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Januari 30, 2026, Ulega amesema kwa sasa wataalamu wa pande zote wanakutana katika mafunzo maalumu yanayotengeneza dira ya nini kitaenda kutokea kupitia mkakati huo kabambe.
“Tunashirikiana na wenzetu kutoka Korea Kusini ambao tayari wamepiga hatua kubwa katika eneo la miundombinu ya barabara. Leo nimefungua mkutano wa mafunzo ambao wataalamu wetu wa Korea wanakutana kuangalia utekelezaji wa mradi huo ili kutoa mafunzo kwa watu wetu,” amesema.
“Lengo letu kupitia mafunzo haya, wataalamu wetu watapata ujuzi utakaowawezesha kujua namna ya kupanga, kutekeleza na kuendesha miradi mikubwa ya barabara.”
Amesisitiza kuwa Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu yake usafirishaji ili iendane na wakati na mahitaji halisi ya wananchi.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza kwenye mkutano uliohusisha wataalamu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na viongozi wa Shirika la Ushirikiano la Korea (KOICA) leo Ijumaa, Januari 30, 2026 jijini Dar es Salaam.
Ulega amesema Serikali imepanga kuhakikisha shoroba zote tisa za barabara nchini zinaunganishwa kwa barabara pana zenye mfumo wa kidijitali, zinazohimili changamoto za kimazingira na zitakazosaidia maeneo ya uzalishaji kuunganishwa na masoko na bandari.
Pia, Ulega ameipongeza Korea kupitia Kampuni ya KOICA kwa uamuzi wake wa kuijengea uwezo Tanzania ili kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa haraka kwa ufanisi,
Waziri Ulega amesema utekelezaji wa hatua hiyo, utatatua changamoto zinazoikabili sekta ya usafirishaji ikiwamo suala la foleni na uchakavu wa miundombinu.
Pia, ametumia nafasi hiyo kuwaasa wataalamu wa sekta ya ujenzi kuhakikisha wanapata ujuzi wa kubuni, kusimamia na kutekeleza ujenzi wa miradi inayoendana na malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2050.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akimsikiliza mtaalamu wa masuala ya ujenzi kutoka Shirika la Ushirikiano la Korea (KOICA) wakati wa kikao kazi kilichohusisha wataalamu wa shirika hilo na wenzao kutoka Wizara ya Ujenzi.
Meneja wa Miradi ya Ubia Kati ya Sekta Binafsi na Serikali (PPP), Elibariki Mkumbo amesema hivi karibuni wataanza utekelezaji wa mradi wa mpango kabambe wa usafiri wa haraka kati ya Kibaha na Morogoro, hatua itakayoleta mapinduzi makubwa katika maboresho ya miundombinu ya usafirishaji nchini.