Pedro awatangazia vita Ahly, wenyewe wajibu

Yanga itakuwa na mchezo mgumu kesho dhidi ya Al Ahly, huku kocha Pedro Goncalves akitangaza kwamba wapo tayari kucheza na mabingwa hao wa kihistoria wa Afrika.

Yanga itakuwa mwenyeji wa Ahly kwenye mchezo wa nne wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa kesho katika Uwanja wa New Amaan.

Akizungumza kwenye mkutano wa maandalizi ya mchezo huo, Pedro amesema kama ingekuwa leo inapigwa mechi hiyo kikosi chake kipo tayari.

Amesema timu imefanya maandalizi uwanjani na hata nje ya uwanja, ambapo wamejipanga kutafuta pointi tatu  mbele ya Al Ahly.

“Tumekuwa na mazoezi ya uwanjani, lakini pia kule hotelini tumekuwa tunafanya vikao na wachezaji wote na mchezaji mmoja mmoja. Kama mechi ingekuwa inatakiwa kuchezwa leo tungekuwa tayari,” amesema Pedro

“Tunakwenda kucheza na timu bora ambayo ina historia kubwa ya mafanikio. Tunajua kwamba tulipoteza kwao, tunataka kucheza kwa nidhamu mchezo wa kesho kwa kila idara ili tushinde.”

Wakati Pedro akisema hivyo, mwenzake wa Al Ahly, Jesse Thorup amesema wanalenga kushinda mechi, lakini wanatambua kwamba watakutana na upinzani mkubwa. 

Thorup amesema Yanga ni timu nzuri yenye wachezaji wenye ufundi, lakini kikosi chake kitaingia na hesabu za kucheza kwa falsafa ya kushinda.

“Hatutakuwa na mchezo rahisi. Tunajua tunaongoza kundi, lakini tunataka kukaa eneo bora zaidi kwenda hatua inayofuata,” amesema Thorup.

“Tunajua kwamba wapinzani wetu wana timu nzuri, wana wachezaji wenye ufundi na ubora mkubwa kitu muhimu hapa ni sisi kucheza soka letu ili tushinde.”