Polisi Mbeya yamshikilia katibu wa Chadema Rungwe, yataja sababu

Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linamshikilia Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Wilaya ya Rungwe, Award Karonga kwa tuhuma mbalimbali za kijinai ikiwamo uchochezi.

Karonga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa hamasa Taifa wa Chama hicho, anadaiwa kukamatwa jana Januari 30 katika maeneo ya mtaa wa Katumba Kata ya Ibighi-Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Jeshi mkoani humo, Benjamin Kuzaga imeeleza kuwa kiongozi huyo anashikiliwa kwa tuhuma mbalimbali za kijinai ikiwamo uchochezi.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa mtuhumiwa alikamatwa saa 4 asubuhi katika mtaa wa Katumba, ambapo upepelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limemkamata na kumshikilia Award Karonga mkazi wa Katumba ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Rungwe na Makamu Mwenyekiti hamasa wa Chama hicho Taifa kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo uchochezi”

“Mtuhumiwa alikamatwa Januari 29 katika Mtaa wa Katumba wilayani Rungwe saa 4 asubuhi na upelelezi unakamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake” imeeleza taarifa hiyo.

Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale amesema wamepata taarifa za kushikiliwa kwa kiongozi, akieleza kuwa imekuwa ni mwendelezo wa kamatakamata ya viongozi wao bila utaratibu.

“Baada ya kushikiliwa alipekuliwa nyumbani kwake huko Tukuyu na baadaye akaletwa kituo kikuu cha Polisi kati na muda huu familia yake, ndugu, jamaa na marafiki na sisi viongozi tupo hapa kufuatilia,” amesema.

“Tumeonana naye lakini bado hatujajua sababu za yeye kushikiliwa, tunalaani vitendo hivi vya mara kwa mara kukamatwa viongozi wetu, ikumbukwe huyu ni kiongozi wa hamasa Taifa,” amesema Mbeyale.