RC Songwe apiga marufuku uchomaji mkaa

Songwe. Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Jabir Makame ametangaza marufuku ya ukataji holela wa miti katika mkoa huo akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaokiuka agizo hilo.

Makame ameyasema hayo wakati wa kuhitimisha Jukwaa la Wadau wa Mazingira, Maji na Nishati Safi ya Kupikia lililofanyika leo Januari 30, 2026, likiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka serikalini na sekta binafsi.

Makame amezitaka mamlaka zote zinazohusika na uhifadhi wa misitu kuandaa mkakati kabambe kwa kushirikiana chini ya usimamizi wa kamati za usalama za wilaya, kwa lengo la kufanya oparesheni za kuwaondoa wavamizi kwenye misitu ili ibakie salama, kulinda vyanzo vya maji pamoja na kuimarisha elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi.

Makame amezisisitiza mamlaka za mazingira uwekaji mikakati madhubuti ya kudhibiti uvamizi wa misitu, ikiwemo ufuatiliaji wa mara kwa mara, utekelezaji wa sheria na ushirikishwaji wa jamii ili kuhakikisha misitu inaendelea kubaki salama kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Katika hotuba yake, Makame amewahimiza wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, na badala yake kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira pamoja na vyanzo vya maji.

Amesema uharibifu wa mazingira unaathiri moja kwa moja upatikanaji wa maji pamoja na ustawi wa jamii, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika kulinda misitu.

“Nitoe wito kwa mamlaka husika ikiwemo TFS, REA, Halmashauri na Kamati za Usalama kuhakikisha sheria na kanuni za uhifadhi wa mazingira zinasimamiwa kikamilifu, sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za nishati safi ya kupikia,” amesema.

Wadau walioshiriki jukwaa hilo wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza mikakati ya uhifadhi wa mazingira, kuboresha huduma za maji na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ili kuifanya Songwe kuwa mkoa wa kijani na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Mmoja wa wadau, Magdalena Simbeye amepongeza uandaaji wa jukwaa hilo ambalo limebadilisha taswira ya uhifadhi wa mazingira kwani usimamizi wa sheria za mazingira hazitekelezwi kama inavuotakiwa hali ambayo imepelekea maeneo mengi kubaki majangwa.

“Endapo sheria za kulinda mazingira zikatekelezwa itapelekea wananchi kuacha kupikia nishati safi na kujikita kutumia nishati safi ya kupikia kama ajenda ya serikali inavyosimamiwa hivi sasa,” amesema Simbeye.

Kwa upande wake, Zakaria Mwampashi amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia inaenda sambamba na uhifadhi wa mazingira hivyo serikali ipunguze gharama za ununuzi wa gesi kwa lengo la kumrahisishia kutumia nishati safi ya kupikia ili tuondokane na matumizi ya nishati chafu ambayo ni mkaa hali itakayoondokana na ukataji miti hovyo.