TCRA: Tuwaandae vijana kuchochea mfumo wa kidijiti

Arusha. Ili kuongeza wataalamu wa usalama wa mtandao watakaolinda mustakabali wa mazingira ya kidijitali nchini yenye kuchochea mfumo wa kidijiti na ubunifu, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeeleza muhimu wa kuongeza jitihada za kuwaandaa vijana katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa Tehama kutoka TCRA, Tusajigwe Mwalukasa amesema ni muhimu jitihada hizo kuongezwa ili kuchochea bunifu na vumbuzi ambazo zitasaidia kubuni suluhu dhidi ya vitisho vya mtandaoni.

 Mkurugenzi huyo ameyasema hayo jana Alhamisi Januari 29, 2026 wakati wa hafla ya shindano la sita la masuala ya usalama mtandaoni lijulikanalo kama Cyber Champions 2025/ 2026, lililofanyika jijini Arusha.

Akizungumza na washiriki hao kutoka vyuo vikuu na vya kati hapa nchini, mkurugenzi huyo amesema ni muhimu kuwa na maandalizi ya kutosha ili kuwa na wataalamu wenye kufanikisha uchumi wa kidijiti.

Amesema intaneti imekuwa uti wa mgongo wa uchumi wa kidijiti kwa kurahisisha utoaji wa huduma za Serikali, kuimarisha shughuli za kijamii na kuchochea ubunifu na uvumbuzi, hali inayochangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na ustawi wa jamii.

“Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, matumizi ya Tehama yameambatana na ongezeko la matishio ya usalama mtandaoni, ikiwemo udukuzi, uvujaji wa taarifa na mashambulizi dhidi ya mifumo ya kidijiti,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Mashindano haya tuliyaanzisha kwa lengo la kuibua vipaji, kuelimisha na kujenga kizazi kijacho cha wataalamu wa usalama wa mtandao kutoka vyuo vya elimu ya juu.

Mkurugenzi huyo amesema sekta ya mawasiliano nchini imeendelea kukua kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni, huduma za simu na intaneti zimeendelea kuwafikia Watanzania wengi zaidi, mijini na vijijini na kuwa hadi kufikia Desemba 2025, idadi ya watumiaji wa intaneti imefikia watu milioni 58.1.

Wanafunzi 50 kutoka Vyuo Vikuu na Kati nchini,wakishiriki shindano la  sita la masuala ya usalama mtandaoni la Cyber Champions,jana jijini Arusha, yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).



Akizungumzia mashindano hayo, amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2025/26, jumla ya vijana 4,285 wameshiriki, kati yao 3,705 ni wavulana, sawa na asilimia 86.47 na 580 ni wasichana, sawa na asilimia 13.53 ambapo kwa mwaka huu washiriki walikuwa 1,226 kutoka vyuo 29 nchini.

Meneja wa TCRA Kanda ya Kaskazini, Mhandisi Francis Mihayo amesema nusu fainali na mashindano hayo ilifanyika Januari 17, 2026 iliyoshirikisha washiriki 465 ambapo kati ya hao, washiriki 50 ndiyo walifuzu kuingia fainali ambapo kati yao wanne ndiyo wameshinda.

Amesema shindano hilo maalumu la kitaifa kwa wataalamu wa masuala ya mitandao limekuwa likikutanisha wanafunzi hao kwa lengo la kuibua vipaji, kutoa elimu na kujenga kizazi cha wataalamu wa usalama wa mtando kutoka vyuo hivyo ambao wataweza kulinda mustakabali wa mazingira ya kidijitali nchini Tanzania.

“TCRA inaendesha hili shindano kwa sababu kuandaa wataalamu ambao wanaweza kusihindana kitaifa na kimataifa na wanne walioshinda kati ya 50, wataendelezwa na kuhakikisha wanaenda kushindani nchi mbalimbali, mwitikio wa mwaka huu umezidi kuwa mkubwa tunaamini mwakani wataongezeka pia,” amesema.

Mmoja wa washindi hao kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Helidorice Mwalongo amesema moja ya sababu zilizomfanya ashiriki mashindano hayo mwaka huu ni kutokana na wasichana wengi kutokujitokeza kushiriki.

“Niliangalia mashindano yaliyopita, wasichana wanaojitokeza ni wachache ndiyo maana mwaka huu nikajitosa, niwaombe vijana hasa wasichana tusiogope kushiriki mashindano haya licha ya kuwa ushindani ni mkubwa ila tujitokeze, tusiogope tukiamua tunaweza,” amesema.

Naye Mkuu wa Kitivo cha Tehama kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Edson Lubua amesema ili Taifa lifikie kwenye mafanikio makubwa katika nyanya hiyo ni lazima waendelee kuwekeza kwa vijana.

“Lazima tuwekeze kwa vijana ili taifa lifikie mafanikio tunayoyataka, teknolojia inazidi kukua hivyo ni muhimu kundi hili kutoliacha nyuma katika masuala ya usalama mtandaoni, ninaamini watakuwa mabalozi wazuri wa usalama wa kidijiti mtandaoni,” amesema.