Wanawake wanapochagua ukimya kuokoa afya ya akili

Alikuwa amezoea kuamka na simu mkononi. Kila taarifa, ujumbe na hata picha aliyoweka kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa sehemu ya maisha yake ya kila siku.

Lakini siku moja, aliamua kuifunga simu, kuondoka mtandaoni.Aliyafanya haya si kwa sababu hakupenda tena dunia ya kidijitali, bali kwa sababu dunia hiyo ilikuwa imemgeuka.

Asha si jina halisi ni binti umri wa miaka 27, mhitimu wa chuo kikuu, mwenye ndoto kubwa na sauti iliyokuwa ikisikika kupitia mitandao ya kijamii.

Binti huyu mkazi wa Buza mkoani Dar es Salaam alikuwa akitumia majukwaa hayo kuzungumzia masuala ya jamii, haki za wanawake na kujitambua. Lakini kadri sauti yake ilivyozidi kusikika, ndivyo mashambulizi yalivyozidi kuongezeka.

“Kulikuwa na siku niliamka na kukuta zaidi ya ujumbe 200 wa matusi.Wengine waliniambia ninyamaze kwa sababu mimi ni mwanamke, wengine walinidhalilisha kwa maneno ya ngono, na baadhi walinitishia.”

Kwa Asha, mitandao ya kijamii ilianza kama jukwaa la fursa. Lakini polepole, iligeuka kuwa uwanja wa vita.

Kila chapisho liligeuka kuwa sababu ya kushambuliwa, picha zake zilichukuliwa na kuhaririwa, maneno yake yalipotoshwa, na utu wake ulivunjwa hadharani.

Alijikuta akiishi kwa hofu, alihofia kuweka chochote, kusoma maoni, na hatimaye hofu ya kuwa yeye mwenyewe.

Simulizi ya Asha si ya kipekee. Ni taswira ya wanawake wengi nchini na duniani kote wanaokumbana na unyanyasaji wa mtandaoni udhalilishaji, lugha ya matusi, vitisho, na mashambulizi ya kijinsia hadi kufikia hatua ya kujiondoa kabisa kwenye majukwaa ya kijamii.

Wengi wao huchagua ukimya si kwa sababu hawana cha kusema, bali kwa sababu gharama ya kusema imekuwa kubwa mno.

“Nilianza kujiuliza, thamani ya uwepo wangu mtandaoni ni ipi kama kila siku ninalia?” Asha anasema.

Usingizi wake ulipotea, hamu ya kazi ikapungua, na afya yake ya akili ikaathirika. Alianza kujitenga na marafiki, akihofia hata kuulizwa maswali rahisi.

Uamuzi wa kuondoka mitandaoni haukuwa rahisi. Ilikuwa kama kukata kiungo kilichokuwa sehemu ya maisha yake. Lakini ulikuwa uamuzi wa kujilinda.

“Nilijiona nimeshindwa, kama nimewapisha waliokuwa wakinidhalilisha.Lakini baadaye nilitambua kuwa nilikuwa najinusuru.”

Kwa Asha, maneno yalikuwa silaha. “Walijua pa kuniumiza.Walijua jamii inawahukumu wanawake kwa vigezo vikali zaidi.”

Kila tusi lilikuwa kama ukumbusho kwamba nafasi ya mwanamke katika anga ya kidijitali bado ina mipaka isiyoonekana lakini inayouma.

“Nimejifunza kuwa haki yangu ya kusema haipaswi kunigharimu afya yangu ya akili, hata hivyo suluhisho si wanawake kuondoka mitandaoni, bali mazingira ya mitandao kubadilika. Kwa nini mimi niondoke, na si wale wanaodhalilisha wawajibishwe?”

Asha bado yuko mbali na mitandao ya kijamii. Lakini ukimya wake una ujumbe mzito. Ni kilio kisicho na sauti kinachowakilisha maelfu ya wanawake waliolazimika kujificha ili kuishi kwa amani.

Simulizi ya Asha inaacha maswali mengi kubwa likiwa Je, anga ya kidijitali ni salama kwa wanawake, au ni kioo kinachoakisi udhalilishaji uliokita mizizi katika jamii?

Mashambulizi kwa wanawake

Wanaharakati wa haki za kidijitali wanakubaliana naye. Wanasema kunahitajika sera madhubuti za kulinda watumiaji, elimu kwa jamii kuhusu matumizi salama ya mitandao, na mifumo ya haraka ya kushughulikia malalamiko ya unyanyasaji.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) Dk Rose Reuben anakiri kuwa kuna ongezeko kubwa la mashambulizi dhidi ya wanawake kwenye mitandao hasa miaka ya karibuni huku wanasiasa, wasanii, wafanyabiashara na watu maarufu wakiwa waathirika wakubwa.

Anasema mashambulizi hayo hayalengwi kwa wanawake bali hata wanaume wanakutana na unyanyasaji huo na kwa bahati mbaya wanaofanya hivyo ni wanawake na wanaume.

“Hali inazidi kuwa mbaya kwa sababu sasa hivi wafanyaji wa vitendo hivi viovu ni wanawake kwa wanaume, hakuna wa kumnyooshea mwenziwe kidole ila ukweli ni kwamba wanaumiza watu wengi ikiwemo huyo binti aliyelazimika kujiweka kando na mitandao.

Tunachofanya Tamwa ni kuwasaidia waathirika wa ukatili ikiwemo huu wa mtandaoni, tuna kitengo cha ushauri nasaha chenye watu wenye uwezo mkubwa wa kunasihi na kutoa ushauri. Mtu aliyekutana na ukatili wa aina hii ni lazima atakuwa ameathirika kisaikolojia hivyo ni muhimu kupata ushauri ili kuweka akili yake sawa kwanza kabla ya hatua nyingine,” anasema Dk Rose.

Mkurugenzi huyo anasisitiza kwa jamii kuweka nguvu kwenye elimu ya matumizi sahihi ya mitandao na ulinzi wa taarifa.

“Kukosekana kwa elimu ya kutosha kwenye ulinzi wa taarifa binafsi na matumizi ya mitandao ya kijamii kunachochea matukio ya aina hii kushika kasi. Imefika wakati kila Mtanzania ni muhimu awe na elimu na ufahamu wa kutosha kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii na ulinzi wa data,”.

Hata hivyo, Dk Rose anasema wanawake kujiweka kando na matumizi ya teknolojia sio suluhu la vitendo hivyo viovu kwa sababu dunia sasa ipo kiganjani.

Anasema: “Maisha ya dasa ni kutembea na teknolojia sasa ukisema ujitoe kwa sababu ya mashambulizi upo uwezekano ukabaki nyuma na kuna fursa ukazipoteza ndiyo maana tunasisitiza unachotakiwa kuwa nacho ni elimu sahihi ya matumizi ya hiyo teknolojia na pale inapotokea umetikiswa ukatikisika usisite kuwaona wataalamu na mamlaka husika kwa hatua zaidi,”

Wanaharakati wa haki za mitandaoni wanasema kukomesha unyanyasaji wa mtandaoni, hususan unaowalenga wanawake, kunahitaji hatua za makusudi kutoka ngazi ya mtu mmoja mmoja hadi taasisi na serikali.

Mwanaharakati wa haki za kidijitali, Neema Mushi, anasema kinachompata Asha kinawakumba wanawake wengi wanaothubutu kutumia mitandao kama jukwaa la kujieleza.

“Wanawake wanapozungumza masuala ya jamii au haki zao, hushambuliwa si kwa hoja bali kwa jinsia yao. Unyanyasaji huu unawalenga moja kwa moja utu na afya ya akili,” anasema.

Neema anasema kukabiliana na hilo Serikali inapaswa kuweka na kusimamia sheria mahususi zinazotambua unyanyasaji wa mtandaoni kama kosa la jinai, ikiwemo vitisho, udhalilishaji wa kingono na matumizi mabaya ya taarifa binafsi.

“Sheria hizo ziwe na adhabu zinazoogopesha ili kuwafanya wanyanyasaji wawajibike. Pia elimu ya uraia wa kidijitali itolewe kuanzia ngazi ya shule hadi jamii kwa ujumla, ikisisitiza heshima, uwajibikaji na athari za maneno mtandaoni. Elimu hii iwafikie pia wazazi na walezi ili waweze kuwaongoza watoto wao.

Mtetezi wa haki za wasichana Zubeda Ndipo anasema kunahitajika mabadiliko ya mtazamo kukubali kuwa wanawake wana haki sawa ya kuwepo, kuzungumza na kusikika bila hofu.

“Wataalamu wa masuala ya kijamii wanasema unyanyasaji wa mtandaoni kwa wanawake una mizizi katika mfumo dume na ukosefu wa uwajibikaji kwenye majukwaa ya kidijitali.

“Mwanamke anapothubutu kuzungumza, kutoa maoni au kujionyesha hadharani, mara nyingi hukabiliwa na mashambulizi yanayolenga jinsia yake, mwili wake na heshima yake”.

Kwa upande wake Badru Shekilongo anasema ipo haja kwa majukwaa na mitandao ya kijamii kuboresha mifumo ya kuripoti unyanyasaji, kuchukua hatua za haraka dhidi ya akaunti zinazokiuka maadili, na kuweka uwazi kuhusu namna malalamiko yanavyoshughulikiwa. Usalama wa mtumiaji upewe kipaumbele kuliko idadi ya watumiaji au faida.