Wawili sekondari za kata waula ufadhili Samia Scholarship kujinoa na AI

Dar es Salaam. Wanafunzi wawili waliohitimu kidato cha sita kwenye sekondari za kata ni miongoni mwa wanafunzi 50 waliopata ufadhili wa masomo wa Samia Scholarship Extended DS/AI.

Wanafunzi hao ni kutoka Magamba sekondari ya Tanga na Sengerema sekondari ya Mwanza ambao walifanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha sita katika matokeo yaliyotoka Julai, mwaka jana.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuliaga kundi la kwanza la wanafunzi 16 wanaokwenda kuanza masomo kwenye Chuo Kikuu cha Johannesburg,  Afrika Kusini kupitia ufadhili huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema  mchakato wa ufadhili huo utaendelea kwa kuzingatia kigezo cha ufaulu mzuri bila kujali umetoka shule gani.

Amesema kati ya wanafunzi 50 waliopata ufadhili huo, wawili wametoka shule za sekondari za kata, akizitaja kuwa ni Magamba Tanga na Sengerema  ya Mwanza.

Amesema vigezo vilivyotumika hadi vijana hao 50 kupata ufadhili huo ni ufaulu mzuri kwenye masomo ya sayansi, ambapo walichukua mwanafunzi wa kwanza hadi wa 50.

Amesema kati yao,  wanafunzi 20 wametoka shule za serikali na wanafunzi 30 wametoka shule za binafsi.

“Habari njema ni kwamba katika ufaulu huu, tumepata wanafunzi wawili waliotoka kwenye shule za kata, hii  imethibitisha hakuna atakayechukuliwa nje ya kigezo cha ufaulu mzuri

Akitolea mfano alivyopigiwa simu na rafiki yake ambaye aliomba kijana wake aingizwe kwenye ufadhili huo, Mkenda amesema hata angekuwa mtoto wa nani kama hajakidhi kigezo cha ufaulu mzuri hawezi kupata ofa hiyo ya kimasomo.

“Nilimwambia huyo rafiki yangu sina cha kukusaidia zaidi ya kumtaka amwambie kijana wake afaulu vizuri na hivi ndivyo itaendelea kuwa kwenye ufadhili huu,” amesema.

Amesema kundi la kwanza la wanafunzi 16 linatangulia Afrika Kusini kuanza masomo wakati kundi la pili la wanafunzi 34 likitarajiwa kujiunga na chuo kikuu cha Limerick kilichopo nchini Ireland.

Mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia, Dk Amos Nungu amesema wanafunzi waliopata ufadhili huo ni wale wa umahiri wa data sayansi na akili unde.

Amesema kwa kuwa wanafunzi hao wametoka shuleni moja kwa moja baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka jana, hivyo  walipelekwa kufundishwa mambo mbalimbali kwenye Chuo Kikuu cha Nelson Mandela jijini Arusha tangu Septemba 15, 2025 kabla ya kuondoka nchini kwenda kuanza masomo yao ya Chuo Kikuu.

Wanafunzi hao wataondoka nchini Februari Mosi kwenda Afrika Kusini kuanza masomo yao katika umahili wa Data Sayansi na akili unde kwenye Chuo Kikuu cha Johannesburg huku 34 waliosalia wakitarajiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Limerick kilichopo Highlands.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, wanafunzi wanufaika wa ofa hiyo, Saimon Aswile na Malaika Florence wamesema walitokea mbali kuanzia kidato cha sita hadi kupata ufadhili huo wa kimasomo. hiyo.

Malaika Florence amesema wako tayari kwenda kusoma, wakiomba Watanzania waendelee kuwaamini.

“Tuna matarajio makubwa katika hatua hii ambayo haikuwa rahisi tangu tukiwa kidato cha sita hadi kupata ufadhili huu, tuko tayari kwenda kusoma,” amesema.

Mnufaika mwingine, Saimon Aswile aliwashauri vijana walipo shuleni kusoma kwa bidii akibainisha nafasi waliyoipata imetokana na matokeo ya ufaulu wao na siyo vinginevyo.