ZAIDI YA BILIONI 67 ZAPITISHWA KUING’ARISHA CHATO

…………

CHATO

BARAZA la Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita, imejadili na kupitisha makisio ya bajeti ya Tsh. Bilioni 67,016,792,267.93 kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na halmashauri hiyo.

Bajeti hiyo inaongezeko la kiasi cha Tsh. 397,666,268 ukilinganisha na makisio ya kiasi cha bilioni 66,619,125,999.93 ya bajeti ya mwaka 2025/26.

Hatua hiyo inaonyesha wazi matamanio ya halmashauri katika kuinua uchumi wa jamii na kukamilisha baadhi ya miradi vipolo ambavyo havikukamilika kwa kipindi cha bajeti ya mwaka jana.

Akizungumza katika kikao cha Baraza hilo maalumu, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mandia Kihiyo, amesema mpango huo wa bajeti umezingatia vipaumbele vya maendeleo kwa kata 23 za wilaya hiyo kwa lengo la kuchochea maendeleo kwa kasi kubwa ukilinganisha na mwaka jana.

Aidha katika mpango huo wa bajeti, wadau mbalimbali wa maendeleo wanatarajiwa kuongeza uchechemuzi wa miradi ya umma, serikali kuu na mapato ya ndani.

Akiwasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji, Ofisa mipango wa halmashauri hiyo, Maria Ndohelo, amesema malengo ya bajeti hiyo ni kutekeleza miradi ya kimkakati na ile muhimu kwa ukuaji wa uchumi.

Kwamba halmashauri hiyo inakusudia kukusanya mapato ya ndani kiasi cha Tsh. 5,757,241,268.00 huku nguvu za wananchi zikikadiliwa kuwa Tsh. 600,000,000.00, fedha kutoka serikali kuu na wahisani ikiwa ni Tsh. 61,259,550,999.93, ruzuku ya mishahara (PE) 38,908,208,000, ruzuku ya miradi ya maendeleo Tsh. 19,835,108,999.93 na matumizi mengineyo (OC) Tsh. 1,916,234,000.00.

Kutokana na hali hiyo, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Christian Manunga, amewahakikishia madiwani hao kuwa bajeti iliyojadiliwa na kupitishwa na Baraza hilo itakwenda kuondoa changamoto za wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa umma.

Kadhalika amedai matamanio yake ni kukusanya zaidi ya bilioni 9 kutoka vyanzo vya ndani vya halmashauri hiyo ili kuvuka lengo la bilioni 5.7 zilizokadiliwa kukusanywa kwa bajeti ya mwaka 2026.

Hata hivyo, kwa kauli moja Baraza la Madiwani hao limepitisha kwa kauli moja makisio hayo na kusisitiza njia bora za ukusanyaji mapato ya halmashauri ili kutekeleza kwa wepesi miradi iliyokwama katika bajeti ya mwaka jana