Azam yaliamsha, Wakenya wakijipanga CAFCC

AZAM imepanga kuendeleza ubabe mbele ya Nairobi United kwenye mchezo wa nne wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika huku Wakenya hao wakija na hesabu zao.

Kocha wa Azam, Florent Ibenge baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza hatua ya makundi ugenini, amesema wanataka kutafuta ushindi wa pili ili kujiweka sawa.

Ibenge amesema hakuna matokeo mengine yatakayokuwa sahihi kwao zaidi ya kuwafunga tena Nairobi United, kwenye mchezo huo utakaopigwa kesho Jumapili saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex hapa Zanzibar.

“Wakati tunaanza mechi hizi za makundi, tulikuwa na malengo ya kushinda mechi zetu tatu za nyumbani, bahati mbaya tukapoteza wa kwanza dhidi ya Wydad,” amesema Ibenge.

“Bahati nzuri kwetu ushindi wetu wa kwanza tumeupata ugenini lakini umetuimarisha, sasa tunataka kushinda hizi mbili za nyumbani tulizobakiza.

“Tunafahamu haitakuwa rahisi, tunakutana na timu ambayo inaweza kubadilika, hatutaki kurudi nyuma tena, tumejiandaa kushinda kwenye mchezo huu wa kesho.”

Wakati Ibenge akisema hayo, kocha wa Nairobi United, Salim Ramadhan amesema kikosi chake licha ya kupoteza mechi tatu za kwanza, bado wataendelea kujipanga kutafuta ushindi wa kwanza.

Ramadhan amesema timu hiyo haiwezi kukata tamaa kwa kuwa bado nafasi wanayo ya kutafuta nafasi za juu.

“Tumekuwa na matokeo mabaya lakini kiwango chetu kimekuwa tofauti, naamini tunaweza kubadilika, tutaendelea kutafuta ushindi kwenye mechi zilizosalia,” amesema Ramadhan.

“Changamoto yetu kubwa tumekuwa na wachezaji ambao wanapata uzoefu lakini tunajivunia namna wanavyoendelea kuimarika na hatutaki kukata tamaa.”