Dar es Saalam. Uvumilivu, subira na bidii ni nguzo kuu za mafanikio katika biashara. Huu ndio ujumbe mzito unaotolewa na mfanyabiashara mkongwe na Mwenyekiti wa Bakhresa Group of Companies, Said Salim Bakhresa, kwa vijana wanaoingia kwenye ujasiriamali na mara kadhaa kujikuta wakikata tamaa wanapokutana na vikwazo vya mwanzo.
Bakhresa, ambaye ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa barani Afrika, amesema mafanikio hayaji kwa mkupuo wala kwa haraka kama wengi wanavyotarajia.
Amewakumbusha vijana kuwa safari ya maisha, hususan ya biashara, ni ndefu na imejaa changamoto ambazo haziwezi kuepukika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kipindi cha Fahari Yetu kinachorushwa na UTV jana Ijumaa Januari 30, 2026, mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 78 amesimulia safari yake ya maisha ilivyoanzia katika mazingira magumu hadi kufikia kilele cha mafanikio ya kibiashara.
Amesema hali ngumu ya maisha ya familia yake ilimlazimu kuacha shule akiwa na umri wa miaka 14 na kuamua kuingia kwenye ujasiriamali ili kusaidia kujikimu.
“Nilianzia kuuza urojo na mishkaki. Ilikuwa ni biashara ndogo ya chakula, lakini niliamini kuwa ni biashara nzuri. Hata nilipoamua kuondoka Zanzibar na kuja upande wa pili wa nchi, niliendelea na wazo la kuanzisha mgahawa, japokuwa mambo hayakuwa rahisi hata kidogo,” amesimulia Bakhresa.
Kutokana na mwanzo huo mdogo, Bakhresa amekua na kujenga himaya kubwa ya biashara inayojumuisha zaidi ya kampuni 17 zinazofanya shughuli zake Tanzania na katika nchi tisa barani Afrika, zikiwamo Kenya, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zimbabwe, Msumbiji, Malawi na Afrika Kusini.
Kwa mujibu wake, siri ya mafanikio yake haikuwa bahati, bali ni uamuzi wa makusudi ya kutokata tamaa licha ya vikwazo vilivyokuwa vinamkabili.
Amesema hakuna mafanikio yanayopatikana kwa urahisi na kwamba changamoto ni sehemu ya maisha ya kila binadamu.
“Maisha ni mwendo mrefu. Misukosuko haikwepeki. Ukiishi duniani lazima utakutana na changamoto. Hakuna kitu cha kuanza leo halafu kesho ukafanikiwa.
“Vijana wasitarajie maisha makubwa kwa haraka. Mambo yanakwenda hatua kwa hatua, kilicho muhimu ni kuweka jitihada na kuendelea kusonga mbele,” amesisitiza.
Bakhresa amekumbuka kuwa,wakati anaingia kwenye biashara, mazingira hayakuwa rafiki kwa wajasiriamali binafsi kwani sekta nyingi za kiuchumi zilikuwa zinaendeshwa na Serikali, hata hivyo, hali hiyo haikumzuia kufuatilia ndoto yake ya kufanikiwa.
“Nilianza biashara katika kipindi kigumu sana. Nilijaribu biashara nyingi, na hakuna biashara ndogo ambayo sikujaribu kuifanya. Nyingi nilizojaribu zilikwama. Mwanzo ulikuwa mgumu kweli kweli, kwa sababu karibu kila nilichojaribu kufanya kilionekana kugonga mwamba,” amesema.
Licha ya kushindwa mara kadhaa, Bakhresa anasema hakuwahi kufikiria kukata tamaa au kurudi nyuma. Badala yake, alichagua kuendelea kujifunza kutokana na makosa na kuongeza juhudi maradufu.
“Sikuwahi kufa moyo. Nilijiambia kuwa safari ni ndefu na inahitaji uvumilivu wa hali ya juu. Nilipitia maisha magumu sana, ndiyo maana nawaambia vijana kuwa kufika hapa si jambo la siku moja au mbili,” amesema Bakhresa.
Kwa upande wake, kazi ilikuwa ndiyo kipaumbele kikuu katika maisha yake, amesema alijituma kwa kiwango cha juu, akitumia karibu muda wake wote kufanya kazi na kuacha kabisa anasa na starehe.
“Muhimu ni kufanya kazi kwa bidii. Mimi nilikuwa nafanya kazi kwa saa 24. Sikuwa na starehe ya aina yoyote. Ilikuwa nikitoka kazini narudi nyumbani. Kuna wakati nilifanya hivyo kwa miezi mitatu mfululizo bila kutoka nje ya ratiba ya kazi na nyumbani. Nilijituma sana, na Mungu akanijalia kufika hapa nilipo leo,” amesema.
Hata hivyo, Bakhresa anakiri kuwa pamoja na juhudi zake binafsi, mchango wa Serikali umekuwa muhimu katika safari ya mafanikio ya kampuni zake.
Amesema mazingira mazuri ya uwekezaji na sera zinazohamasisha biashara yameziwezesha kampuni zake kukua na kupanua shughuli zake ndani na nje ya nchi.
Amesema hakufikiria kampuni yake ingekuwa kwa ukubwa ambao umefikia sasa ila kwa jitihada alizofanya na namna alivyozichangamkia fursa kila alipoziona vimechangia kwa kiasi kikubwa kufikia hatua aliyopo sasa.
Kwa vijana wanaoanza au wanaoendelea na safari ya ujasiriamali, Bakhresa anawasisitiza kuwa subira, nidhamu, bidii na imani ni silaha muhimu ambazo haziwezi kuepukwa katika safari ya kuelekea mafanikio ya kweli.