YANGA imemaliza utata baada ya kumuondoa kiungo Moussa Bala Conte akimpisha winga mpya wa timu hiyo, Buba Jammeh aliyekamilisha usajili wake saa chache kabla ya dirisha dogo kufungwa Januari 30, 2026.
Usajili wa Buba umefanya Yanga kumtoa kwa mkopo Conte kwenda Raja Casablanca ya Morocco inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids.
Winga huyo ambaye ni mapendekezo ya kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, ujio wake ulikuwa lazima ukate jina moja kwenye wachezaji 12 wa kigeni ndani ya timu hiyo na karata ikamuangukia Conte.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga, kimethibitisha taarifa hizo huku kikiweka wazi kuwa tayari kiungo huyo ameondoka Tanzania kuelekea Morocco kwa ajili ya kujiweka sawa na kuanza maisha mapya.
“Ni kweli Conte kaondoka, ilikuwa ni lazima mchezaji mmoja atoke ili usajili mwingine ufanyike, hilo tayari limekamilika. Ni mkopo wa miezi sita, tunaamini mambo yataenda vizuri.
“Mchezaji ameridhia kwenda huko baada ya makubaliano na tayari ameanza safari leo (jana Jumamosi) kwa ajili ya kujiunga na timu hiyo ambayo kocha Fadlu ndio alitoa mapendekezo ya kumuhitaji Conte kwani anamfahamu.”
Mtoa taarifa huyo aliendelea kwa kusema: “Tuliwahusisha makocha, lilikuwa swali rahisi tunamleta Jammeh je atoke nani na kocha akasema ni wakati wa Conte kuachia nafasi.
“Awali tulikuwa na wasiwasi na Assinki (Frank) lakini kocha akasema bado anamtaka kwenye timu Assinki abaki kwa kuwa ana ubora mkubwa na idadi iko sawa.”
Conte amekuwa kwenye presha kubwa ya kuondolewa Yanga kwenye dirisha hili ambapo mapema ilikuwa kama atabaki baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi akiwaacha wenzake Celestine Ecua na Mamadou Doumbia wakiondolewa
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Conte ili kuzungumzia hilo ambapo alithibitisha taarifa hizo na kuweka wazi kuwa anaamini amefanya uamuzi sahihi kutokana na timu aliyekuwepo kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara.
“Ni kweli kuna ofa hiyo na muda wowote naweza kuondoka kwenda kujiunga na Raja Casablanca, ni uamuzi sahihi nilioufanya, naenda kujaribu maisha mengine huko baada ya Yanga kukosa nafasi.
“Hakuna nilichopoteza zaidi nimepata nafasi nyingine ya kwenda kuonyesha na kupambania nafasi ya kuaminiwa ili nipate muda wa kucheza kikosi cha kwanza, kazi yangu ni kucheza, nataka nicheze,” alisema Conte.
Kutua kwa Buba mwenye umri wa miaka 24 ambaye ni raia wa Gambia ingawa pia ana uraia wa Angola ambako ameishi kwa miaka mitano, ulifanya Yanga kuwa na wachezaji 13 wa kimataifa huku kanuni zikiruhusu wawe 12 kwa timu moja, ndipo uamuzi wa Conte kutolewa ukafanyika kama ilivyokuwa kwa Andy Boyeli aliyerudishwa Sekhukhune ya Afrika Kusini, huku pia Mohamed Doumbia naye akipelekwa kwa mkopo Marumo Gallants ya Afrika Kusini, wakati Celesine Ecua naye akipelekwa kwa mkopo JS Kabylie.
Hadi anajiunga na Yanga, Buba ameitumikia Interclube katika michezo saba yote ikiwa ya Ligi Kuu Angola na kufunga bao moja.
Mchezaji huyo anayemudu kucheza winga za pande zote kwa vile ana uwezo wa kutumia miguu yote miwili kwa ufasaha akibebwa na kasi pamoja na chenga za maudhi, pia kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati.
Huyo anakuwa mchezaji wa pili raia wa Gambia kusajiliwa na timu inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, wa kwanza akiwa ni Lamine Jarju aliyepo Singida Black Stars.
Buba anakamilisha idadi ya wachezaji 12 wa kimataifa walipo Yanga hivi sasa ambao ni Djigui Diarra, Kouassi Attohoula Yao, Frank Assinki, Chadrack Boka, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Pacome Zouzoua, Prince Dube, Lasine Kouma, Allan Okello, Dilson Aurélio ‘Depu’ na Buba Jammeh.