Bunge lilivyofunga mjadala hotuba ya Rais, Dk Mwigulu akitoa maagizo

Dodoma. Serikali imetaja maeneo yanayoongoza kwa uvujaji wa fedha za umma na kueleza mikakati inayochukuliwa kuyaziba ikisisitiza kuwa pamoja na changamoto zilizopo, nchi haijasimama bali inaendelea kusonga mbele kimaendeleo.

Kauli hiyo imetolewa kufuatia michango ya wabunge waliotoa maoni yao wakati wa mjadala wa hotuba ya Rais, Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Novemba 14, 2025 wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13, baadhi yao wamesema bado kuna mianya ya upotevu wa fedha za umma huku baadhi ya wahusika wakijificha chini ya mwavuli wa kile kinachoitwa uchawa.

Miongoni mwa wabunge walioibua hoja hiyo ni Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, aliyesema Serikali inapaswa kubana mianya ya upigaji wa fedha za umma kwa kuwa wanaohusika wanajulikana. Shabiby alidai kuwa anayo orodha ya wahusika na kusisitiza kuwa licha ya baadhi yao kuamini wamejificha, jamii inawatambua waziwazi, ikiwemo kupitia majengo wanayomiliki ambayo hata huandika majina yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola, alisema kumekuwa na ufisadi mkubwa unaojificha kwenye kivuli cha uchawa, hali aliyosema haiwezi kuvumiliwa. Lugola alipendekeza kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya uchunguzi ili kudhibiti hali hiyo, huku akilitaka Bunge kuwapa uhuru wawakilishi wake bila kuwabana kupitia vikao vya chama.

Hoja hizo zilihitimishwa katika wiki ya kwanza ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 13, huku kuanzia kesho wabunge watfanya uchaguzi wa wabunge watakaoiwakilisha nchi katika mabunge ya kimataifa kabla ya kuanza mjadala wa Mpango wa Serikali.

Akijibu hoja hizo jana Ijumaa Januari 30, 2026 bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba alisema maeneo makuu yanayochangia upotevu wa fedha za umma ni kwenye ununuzi na makusanyo.

Dk Mwigulu amesema maeneo hayo yanavishawishi na kuna wizi mkubwa na sheria ya manunuzi inapaswa kuangaliwa upya kwa kuwa imekuwa lango la upotevu wa fedha.

“Nchi yetu haijasimama, tunazidi kusonga mbele, lakini ni lazima tuyatazame upya maeneo haya ili kuendana na hotuba ya Mheshimiwa Rais,” alisema Waziri Mkuu huyo.

Aliongeza kuwa kamati za zabuni zinakabiliwa na ushawishi mkubwa, usipodhibitiwa unaweza kuathiri uwajibikaji na malengo ya taifa.

Pia, amewajibu wanaohoji uuzwaji wa dhahabu kwa kuhoji iwapo walitarajia dhahabu hizo zitumike kutengeneza shanga, badala ya kuingiza mapato.

Akichangia mjadala huo, Waziri wa Fedha, Dk Hamisi Mussa Omary alisema ujenzi wa taifa unahitaji ustahimilivu na muda mrefu, huku akibainisha kuwa ndani ya miaka 60 ya Uhuru, Tanzania imepiga hatua licha ya changamoto hasa ikizingatiwa kuwa sasa ina idadi ya watu takribani milioni 71, wengi wao wakiwa vijana.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe alisema katika kipindi kijacho kipaumbele kitawekwa kwenye sekta za elimu, afya na miundombinu.

Amesisitiza kuwa ufuatiliaji wa fedha za umma uanze kwenye halmashauri, huku wenyeviti na mameya wakitakiwa kuitisha vikao vya kamati za fedha kila Jumamosi kwa uwazi zaidi.

Katika sekta nyingine, Mawaziri mbalimbali walieleza mipango ya Serikali ikiwemo ajira mpya 41,500, uboreshaji wa huduma za maji vijijini, sera ya uvuvi wa kisasa, maendeleo ya michezo pamoja na kutenga Sh2 bilioni kwa ajili ya kuwasaidia vijana wanaotengeneza maudhui ya mtandaoni ya kulitangaza taifa.