Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Musoma, imebatilisha na kufuta hukumu ya kifungo cha 30 aliyokuwa amehukumiwa Adolf Hitler baada ya kukutwa na hatia ya kosa la ubakaji.
Hitler maarufu kwa jina la Masiringi alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Butiama mwaka 2023, katika kesi ya ubakaji wa msichana aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha tatu mwenye umri wa miaka 17.
Mrufani alidaiwa kati ya Machi 2022 hadi Agosti 2022, alimdanganya mwanafunzi huyo aondoke nyumbani kwa wazazi wake ili amuoe, ambapo alikamatwa Novemba 12 mwaka huo akiwa na mwanafunzi huyo.
Hukumu iliyomwachia huru Hitler imetolewa Januari 29, 2026 na Jaji Kamazima Kafanabo aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia mwenendo wa kesi hiyo, Jaji amesema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka haukuthibitisha kesi hiyo pasipo kuacha shaka.
Miongoni mwa sababu Mahakama ni pamoja na mwathirika wa tukio hilo kudai tukio hilo lilitokea Ushirombo mkoani Geita wakati hati ya mashtaka ikieleza tukio hilo lilitokea Butiama, mkoani Mara.
Mahakama imesema tofauti hiyo ya kijografia ni ya msingi na haiwezi kurekebishwa kwa maelezo hasa pale ambapo hakuna marekebisho ya shtaka yaliyofanywa na upande wa mashtaka.
Aidha Mahakama ilibaini kuwa muda uliotajwa katika hati ya mashtaka kati ya Agosti 14, 2022 hadi Novemba 12, haukuungwa mkono na ushahidi hivyo ushahidi haikuthibitishwa kuwa alifanya ngono na mwathirika wa tukio hilo katika eneo na muda uliotajwa.
Katika uamuzi wake Mahakama ilirejea maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufaa yaliyowahi kusisitiza kuwa tofauti kati ya shtaka na ushahidi ni kosa la msingi ambali linaweza kuua kesi ya upande wa mashtaka endapo hati ya mashtaka haitarekebishwa.
Kutokana na dosari hizo Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za mrufani kwamba upande wa mashtaka ulitunga mazingira yasiyoendana na ushahidi uliotolewa mahakama.
“Ni jambo lisilopingika kisheria ni kwamba pale ambapo kuna tofauti kati ya hati ya mashtka na ushahidi uliotolewa, bila kufanyika marekebisho yoyote ya shtaka, matokeo yake ni kushindwa kwa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi yake kwa kiwango kinachotakiwa katika mashauri ya jinai,” amesema
Baada ya kuridhia rufaa hiyo, Mahakama ilifuta hukumu hiyo na kuamuru mrufani aachiliwe huru isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine.
Awali mrufani huyo alishtakiwa kwa kosa la ubakaji kinyume na vifungu vya 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Mwaka 2022
Ilidaiwa kwamba katika tarehe tofauti kati ya Agosti 14, 2022 na Novemba 12, 2022, Wilaya ya Butiama katika Mkoa wa Mara, ambapo alidaiwa kuwa na uhusiano na binti huyo.
Hati ya mashtaka ilidai matukio pia linaonyesha kwamba mnamo tarehe 14 Agosti 2022, katika eneo la Biatika ndani ya wilaya ya Butiama katika mkoa wa Mara, Mrufani alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi huyo.
Katika mahakama hiyo ya chini mrufani alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Kutokana na kutoridhika na uamuzi wa Mahakama ya hiyo, mrufani aliwasilisha rufaa hii, akiwa na sababu sita ikiwemo Hakimu wa kesi alifanya makosa kwa kushindwa kuzingatia kwamba umri wa mwathiriwa haukuthibitishwa bila shaka yoyote.
Nyingine ni Hakimu alikosea kumtia hatiani mrufani, kwani haikuthibitishwa bila shaka yoyote kwamba mrufani alitenda kosa la ubakaji, Mahakama ilifanya makosa kwa kutegemea ushahidi usiothibitishwa wa shahidi wa kwanza na wa pili ambao ulikuwa unapingana na wa shahidi wa nne.
Sababu nyingine ni Mahakama ilifanya makosa katika kumtia hatiani mrufani kwa kuwa kesi ya upande wa mashtaka haikuthibitishwa kabisa bila kuacha shaka na ilikosea kuagiza fidia ya Sh3 milioni bila uthibitisho wowote wa hasara yoyote ya kimwili au jeraha la kibinafsi lililompata mwathiriwa.