:::::::
Na WAF, Kagera
Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera Bw. Bwai Biseko ameitaka timu ya wataalam wa kuzuia na kukabiliana na majanga ya dharura katika mkoa wa Kagera ijikite zaidi kutoa elimu ya majanga ya dharura na athari zake kwa ngazi ya jamii ili jamii iweze kutambua dalili na kuchukua tahadhari.
Bw. Bwai ameyasema hayo leo Januari 30, 2026 wakati akihitimisha kikao kazi cha tathmini kuainisha viatarishi vinavyoweza kusababisha athari za kiafya kilichofanyika Mkoani Kagera.
“Tumeweka mpango wa usambazaji wa taarifa za majanga ya dharura kupitia mifumo tofauti, hivyo nisisitize mifumo hiyo izingatie ngazi za jamii ili iweze kusaidia katika kupanga mipango itakayoleta matokeo yaliyokusudiwa” amesema Bw. Bwai
Pamoja na uwepo wa majanga ya magonjwa ya milipuko na ajali za barabarani, Bw. Bwai amesisitiza kuweka kipaumbele katika athari za ajali za majini kwani kama mkoa, wapo kwenye hatari ya kukumbwa na ajali nyingi za majini kwani sehemu kubwa pia ya jamii imejikita katika shughuli za uvuvi.
Katika upande mwingine amewataka wataalam kuweka na kuzingatia mfumo wa matumizi ya takwimu zinazokusanywa katika majanga ili zisaidie katika katika utoaji wa elimu na uratibu wa matumizi wa rasilimali wakati wa kukabiliana na majanga ya dharura kabla na pindi yanapotokea.
Aidha, ameipongeza timu hiyo ya wataalam kwa kazi kubwa ya kufanya tathmini hiyo, huku akiahidi kuwa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa ipo tayari kwa kikao cha uwasilishaji wa taarifa hiyo kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mambo yaliyainishwa na kulinda na kuimarisha hali ya afya katika Mkoa.
Kwa upande wake Mratibu wa Mratibu-Udhibiti wa Athari za Majanga kutoka Wizara ya Afya Dkt Saumu Nungu amesema kuwa kupitia kikao kazi hicho wameweza kuainisha takribani viashiria 17 vinavyoweza kusababisha athari katika afya ya binadamu ikiwemo magonjwa ya mlipuko, ajali za barabarani, majini na anga, uhamiaji haramu, ajali za migodini, tetemeko la ardhi mafuriko na mmomonyoko wa udongo, ambayo kupitia utekelezaji wa mpango kazi ulioandaliwa watakwenda kuzuia, kupunguza na hata kuyakabili majanga hayo.
Naye Mganga wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Samwel Laizer amesema kuwa, kwa kuzingatia utekelezaji wa mpango kazi wa kikao hicho unakwenda kuimarisha na kuhakikisha kuwepo kwa utayari wa kuyazuia na kuyakabili majanga hayo na athari zake, huku ukiimarisha hali ya usalama wa afya za wananchi wa Mkoani Kagera na maeneo jirani dhidi ya majanga hayo.









