Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika kuanzia Novemba 17, 2025.
Matokeo hayo yametangazwa leo Jumamosi Januari 31, 2026 na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Profesa Said Mohammed.
Jumla ya wanafunzi 569,883 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari waliosajiliwa katika shule 5,864 na watahiniwa na kujitegemea wakiwa 25,927 waliosajiliwa katika vituo 813.
naTaarifa ya Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohammed ya Novemba 16, 2025, ilieleza idadi ya watahiniwa wa mwaka 2025 ni ongezeko la asilimia 7.67 ikilinganishwa na wa mwaka 2024.
Kati ya watahiniwa wa shule 569,914 waliosajiliwa mwaka 2025, wavulana ni 266,024 sawa na asilimia 47 na wasichana ni 303,859 sawa na asilimia 53.
Mahudhurio katika mtihani huo yalikuwa asilimia 97.5 sawa na wanafunzi 555,606.
Takwimu zinaonesha kuwa ufaulu umepanda kwa asilimia 2.61 na kufikia asilimia 94.98 ambapo watahiniwa 526, 620 wamefaulu kwa kupata daraja I,II, III na IV.
Ufaulu kwa waliopata daraja la kwanza mpaka la tatu wameongezeka wakiwa wanafunzi 255,404 sawa na asilimia 46.1.