Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha
SERIKALI imesema imejiandaa kutokomeza kabisa migogoro ya ardhi nchini kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid inayotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni Jijini Tanga na baadae kuendelea katika Mikoa mingine.
Akizungumza Jana Januari 30, 2026 Jijini hapa wakati wa kufunga Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kuhusu masuala ya msaada wa kisheria (Mama Samia Legal Aid) katibu Mkuu wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi amesema migogoro ya ardhi imekuwa tatizo kubwa nchini.
“ Katika awamu ya kwanza na ya pili ya zoezi la kampeni ya kutoa msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid, migogoro ya ardhi ilionekana kuwa kinara dhidi ya malalamiko mengi yaliyokuwa yakihitaji msaada wa kisheria,”
“ Kwa kuwa tumegundua hilo ni tatizo kubwa, Serikali hivi sasa tumejipanga kuhakikisha tunatokomeza kabisa migogoro hii na kufanya watu waishi kwa amani,” amesema.
Amesema tofauti na awamu zingine za kampeni hiyo, awamu hii migogoro itakayowasilishwa wataalam wa Sheria watahakikisha wanaifuatilia kuanzia mwanzo hadi mwisho wake Ili isiweze kujirudia kabisa.
Maswi amesema katika mafunzo ya siku tatu Jijini Arusha waliyopewa Mawakili na wanasheria hao wa Serikali ni pamoja na kuhakikisha wanaondokana na rushwa kupitia kampeni hiyo Ili kuweza kutenda Haki Kwa wote.
Amesema Ili kuifanya kampeni hiyo kuwa endelevu na kuipa ngivu zaidi, wizara ya Katiba iliamua kushirikisha mamlaka za Mikoa pamoja na Tamisemi.
Maswi amesema hadi kufikia Juni mwaka Jana 2025, zaidi ya wananchi 4000 waliwasilisha maombi yao katika kampeni hiyo wakihitaji msaada wa kisheria na kwamba miongoni mwa migogoro iliyowasilishwa migogoro ya ardhi ilikuwa ikiongoza.
“ Migogoro iliyofuatia baada ya ardhi ni mirathi na pia changamoto ya ndoa, na ndio sababu tukaamua kuwaita wenzetu wa sekretarieti za Mikoa kwa kushirikiana na Tamisemi na baadae tutaita Halmashauri zote Kwa kuwa Hawa wote ndio wako karibu na wananchi,” amesema.
Amesema kampeni hiyo awali haikuwa ikitatua migogoro hadi mwisho kwa kuwa ilikuwa ikifanyika katika ngazi ya kitaifa lakini hivi sasa migogoro yote itamalizwa Hadi mwisho kwa kuwa itakuwa ikifanyika Kwa ngazi ya Mkoa na Serikali za mitaa
Akifunga mafunzo yaliyodumu Kwa siku tatu Jijini Arusha Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa TAMISEMI Adolf Ndunguru amesema Mawakili hao wapewe mazingira wezeshi ya kufanyia kazi wote walioko katika sekretarieti za Mikoa na wahakikishe wanaviishi viapo vyao Kwa mujibu wa Sheria na miongozo iliyopo.
Aidha amewataka kwa namna yoyote kuepuka vishawishi vya rushwa vinavyoweza kupoteza Haki za wananchi, “ lengo kuu ni kuwarudishia wananchi tabasamu,” amesema na kuongeza:
“”Ikumbukwe kuwa Rais wetu ana nia njema na wananchi wake, ndio maana aliamua kuipa kampeni hii jina lake (Mama Samia Legal Aid) na kufikia mwezi wa sita mwaka Jana wananchi Milioni 4.1 walipata msaada, na tunatarajia kupitia kwenu wananchi wengi waweze kunufaika”amesema.
Kwa upande wake Katibu wa chama cha Mawakili wa Serikali, Wakili Rashid Mohamed Said amesema katika mafunzo hayo wameweza kufanya tathmini ya kampeni nzima iliyokuwa ikitolewa na kujifunza njia mbadala ya kutatua migogoro inayowasilishwa.


