Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limetangaza kuanza msako maalumu wa kuwakamata watu wote wanaotumia Barabara za Mwendokasi (BRT) kinyume cha sheria, likisema kitendo hicho ni miongoni mwa makosa ya usalama barabarani.
limesema licha ya kutoa elimu ya usalama barabarani kwa makundi yote, bado kuna watumiaji wa vyombo vya moto, hususan waendesha bodaboda na mikokoteni, wanakiuka makusudi sheria za usalama barabarani na kuwa chanzo cha ajali.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumamosi, Januari 31, 2026, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jumanne Muliro amesema hatua lazima zichukuliwe sambamba na kutoa onyo kali kwa wote wanaokiuka sheria.
“Hivi sasa kumeibuka tabia ya baadhi ya waendesha vyombo vya moto kupita kwenye barabara za Mwendokasi, jambo linalokwenda kinyume na lengo la Serikali la kuanzisha mfumo wa mabasi yaendayo haraka kwa usafiri salama na wenye ufanisi.Tumejipanga kuanza kusimamia sheria kikamilifu,” amesema.
Muliro amesema Jeshi la Polisi tayari limetoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwamo waendesha pikipiki, mikokoteni, madereva wa magari ya kawaida na mabasi, hatua inayofuata ni utekelezaji wa sheria.
“Kilichobaki sasa ni kuwasimamia kwa karibu, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema.
Amesema waendesha vyombo wanaotumia barabara za mwendokasi hujiweka katika hatari ya kupoteza maisha na pia kusababisha ajali kwa mabasi yanayobeba abiria wengi.
“Dereva wa basi anapojaribu kumkwepa dereva bodaboda anaweza kusababisha ajali mbaya inayohatarisha maisha ya watu wengi kwa sababu ya mtu mmoja au kikundi kidogo kilichokaidi sheria,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kamanda Muliro amesema jumla ya watuhumiwa sita waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya makosa ya jinai wamepatikana na hatia na kuhukumiwa vifungo mbalimbali, ikiwamo vifungo vya maisha jela.
Amesema kesi hizo zilikamilika mwishoni mwa Desemba 2025 na mwanzoni mwa Januari 2026, na zilihusisha makosa ya kubaka, kulawiti, kutorosha wanafunzi pamoja na kuwapa mimba watoto wa shule.
“Mwisho wa Desemba 2025 na mwanzoni mwa Januari 2026, Mahakama zimekamilisha kesi kadhaa za makosa chukizo dhidi ya binadamu, watuhumiwa sita wamepatikana na hatia na kuhukumiwa adhabu kali ikiwamo kifungo cha maisha,” amesema Muliro.
Amesema miongoni mwa waliopatikana na hatia ni Peter Julius, mkazi wa Mbezi Mwisho, aliyefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ubungo na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.
Amemtaja Dunia Salum maarufu kwa jina la Dunia, mkazi wa Chanika, ni mtuhumiwa mwingine aliyefikishwa Mahakama ya Ilala kwa kosa la kubaka na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Rashid Rajabu, mkazi wa Mwanagati, naye alihukumiwa kifungo cha maisha jela na Mahakama ya Ilala kwa kosa la kulawiti.
Muliro amesema upande wa Mahakama ya Temeke, John Jacob Nyamahemba, mkazi wa Mbagala, alihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka, huku Mahakama ya Kigamboni ikimhukumu Abdallah Faustine, mkazi wa Kibada, kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa hilo hilo.
“Mahakama hiyo hiyo ya Kigamboni pia ilimhukumu Abubakari Membe maarufu kwa jina la Abuu kifungo cha maisha jela kwa kosa la kubaka,” amesema.
Akizungumzia uzito wa adhabu hizo, Kamanda Muliro amesema zinatoa funzo kwa jamii na wahalifu kwa jumla, huku akisema wengine bado kesi zao zinaendelea.
“Uzito wa adhabu hizi unaakisi uzito wa makosa yaliyofanywa. Haya ni makosa ya kuchukiza, yanayohatarisha usalama wa jamii na kuvunja maadili ya taifa,” amesema.
Amesema Jeshi la Polisi halitakuwa na huruma kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo.
“Makosa haya ni hatari kwa jamii, na yeyote atakayepatikana na hatia, adhabu yake ni kali kwa mujibu wa sheria. Hatutasita kuchukua hatua za kisheria,” amesema Muliro.