Rufaa yamwokoa mwanajeshi wa DRC aliyehukumiwa kwa unyang’anyi Tanzania

Bukoba. Askari wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Seseko Samilukora aliyekimbilia Tanzania kuwakimbia M23 na baadaye kukamatwa na kufungwa miaka 30 jela kwa unyang’anyi wa kutumia silaha, ameachiwa huru.

M23 ambalo linajulikana kama March 23 Movement au Mouvement du 23 Mars, ni kundi lililojitokeza Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo likiendesha mashambulizi dhidi ya majeshi ya Serikali ya DRC na washirika wake.

Seseko na wenzake wanne wakiwamo wawili ambao ni raia wa Rwanda, walifikishwa kortini kwa mara ya kwanza, Novemba 29, 2024, wakikabiliwa na shitaka la kumpora Fulgence Dawson, Sh10 milioni kwa mtutu wa bunduki.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa ni Rukindo Issa na Ishimwe Clement ambao walikuwa ni Kabendegere Kalisa ambaye alikuwa mshitakiwa wa pili na wa tatu ambao ni raia wa Rwanda na mshitakiwa wa nne, Steven Rusanganwa.

Kupitia hati ya mashitaka, upande wa Jamhuri ulidai tukio hilo lilitokea Novemba 19,2024 eneo la Kimisi Barabara Kuu ya Karagwe-Ngara katika Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato, Wilaya ya Ngara mkoani wa Kagera.

Kabla ya kupora fedha hizo, upande wa mashitaka ulikuwa unadai kuwa kabla au baada ya kupora, watuhumiwa walitumia silaha na visu kumtisha Fulgence.

Warufani katika shauri hilo walikanusha mashitaka hayo na kesi kusikilizwa ambapo upande wa Jamhuri uliita mashahidi wanane  na vielelezo 10 huku washitakiwa wakijitetea bila mashahidi na wengine kulazimika kupewa mkalimani.

Hii ni kwa sababu baadhi ya washitakiwa ambao ni warufani katika shauri hilo walikuwa wakizungumza lugha ya Kinyambo ambayo huzungumzwa zaidi katika Mkoa wa Kagera na baadhi ya maeneo ya nchi za Uganda na Rwanda.

Hata hivyo, katika hukumu ya rufaa, Jaji Immaculata Banzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Bukoba, aliyoitoa Januari 29,2025, aliwaachia warufani hao, akisema Jamhuri ilishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Katika ushahidi wake, Fulgence Dawson ambaye ni mwathirika, alidai kuwa Agosti 19,2024, aliondoka Mtukula kuelekea Dar es Salaam akitumia gari lake aina ya Toyota Wish namba T838 DMC akiwa amewapakiza watu wengine wawili.

Kwenye saa 2:00 asubuhi akiwa anakaribia kizuizi cha mwisho kilichopo Ngara, aliona mti ukiwa umewekwa barabarani na kufunga barabara hiyo, alisimamisha gari na ghafla mtu mmoja akiwa na bunduki alijitokeza na kufyatua risasi hewani.

Muda mfupi baadaye walijitokeza watu wawili nao wakiwa na bunduki wakifuatiwa na wengine ambao baadhi yao walikuwa wamebeba fimbo na kuanza kuvunja vioo ya gari, wao walishuka kwa ajili ya kuokoa maisha yao, wakaamriwa kulala chini.

Baada ya hapo, watu hao walimpekua mifukoni na kuchukua Sh52,000 na kwenye gari walichukua Sh10 milioni na kutoweka.

Alikwenda kwenye kizuizi cha polisi Ngara na kutoa taarifa huku akidai aliwatambua baadhi ya majambazi hao.

Shahidi wa 6 ambaye ni Ofisa wa Polisi, Idrisa Kisaka alieleza kuwa, wakati anafanya operesheni kutokana na tukio hilo, alipokea taarifa fiche kuwa waliofanya tukio hilo walikuwa wanatoka Wilaya ya Kyerwa wakifanya mipango ya kuvamia benki.

Alifanyia kazi taarifa hizo na kuwakamata warufani katika rufaa hiyo na kudai kuwa, katika mahojiano na polisi, walikiri kufanya tukio hilo ambapo waliwapeleka kwa mlinzi wa amani kuandika maelezo ya ungamo ambako nako walikiri makosa.

Maelezo yao ya onyo na yale ya ungamo yalipokewa kama kielelezo kortini.

Katika utetezi wake, mshitakiwa wa tano, Samilukora, alisema yeye ni askari wa Jeshi la DRC na kwamba Oktoba 16,2024 alikimbilia Uganda kuepuka vita na kundi la M23 na kwa sababu ya hofu na kurudishwa vitani, alikimbilia Tanzania.

Alipofika Tanzania alienda moja kwa moja kuripoti Ofisi za Idara ya Uhamiaji na walipobaini yeye ni mwanajeshi, alihamishiwa Dar es Salaam ambako alikaa wiki kadhaa na kurudishwa Kabanga na alishitakiwa kwa wizi wa kutumia silaha.

Kwa upande wake, mshitakiwa wa 4, Rusanganwa alieleza kuwa, alikamatwa Oktoba 24,2024 huko Kyerwa na kupelekwa kambi ya Jeshi inayoitwa Kaisho, huko aliulizwa kama anamfahamu Pendo lakini alikana kumfahamu.

Baadaye alipelekwa kituo cha polisi Kabanga na kufikishwa mahakamani.

Mshitakiwa wa tatu, Ishimwe Clement ambaye ni raia wa Rwanda, alisema alikamatwa Oktoba 20,2024 katika Soko la Isingiro alipokwenda kununua mahitaji, alipelekwa mahali na baadaye alikuja kugundua ni Dar es Salaam.

Alikaa huko kwa wiki tatu huku akiteswa aseme kama yeye ni ofisa wa jeshi, baadaye alisafirishwa na kupelekwa eneo linguine.

Alikaa huko hadi siku alipopelekwa mahakamani na kuunganishwa na washitakiwa wengine.

Mshitakiwa wa pili ambaye naye ni raia wa Rwanda, Issa, alidai alikamatwa Oktoba 20,2024 huko Karagwe akishukiwa kuwa ni ofisa wa polisi na alipelekwa kituo cha polisi kimoja hadi kingine na baadaye kufikishwa kortini.

Kwa upande wake, mshitakiwa wa kwanza, Kalisa alidai kukamatwa Oktoba 20,2024 huko Kyerwa na kupelekwa Dar es Salaam alipokaa wiki tatu huku akiteswa, alikiri kumfahamu mtu anayeitwa Ruzima, lakini aliwaambia hamjui.

Baadaye alisafirishwa hadi kituo cha polisi Kabanga alipokaa mahabusu wiki mbili kabla ya kufikishwa mahakamani, lakini kwa jumla, washitakiwa wote walikana kuandika maelezo ya onyo wala ya ungamo kukiri kutenda kosa hilo.

Hakimu aliyesikiliza shauri hilo alishawishika na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashitaka na kuukataa utetezi wa washitakiwa na kuwahukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, hawakuridhika wakaamua kukata rufaa.

Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, warufani waliowakilishwa na mawakili Peter Matete na Elphace Rweshabura, walitoa sababu 5 wakidai hakimu alikosea kisheria na kimantiki kuwafunga wakati mashitaka dhidi yao hayakuthibitishwa.

Wakili Matete alieleza kuwa maelezo ya onyo na yale ya ungamo yalichukuliwa kinyume cha sheria na kulikuwa na tofauti kati ya maudhui ya hati ya mashitaka na ushahidi uliotolewa kortini na mashahidi wa Jamhuri kuwa ulipishana.

Pia alisema warufani hao walinyimwa haki ya msingi ya kusikilizwa na kutolea mfano wa mshitakiwa wa kwanza anayezungumza Lugha ya Kinyambo pekee kwamba hakupewa mkalimani alipohojiwa polisi wala kwa mlinzi wa amani.

Pia, alisema upande wa Jamhuri ulishindwa kuita mashahidi muhimu, mathalan, watu waliokuwa pamoja kwenye gari na mlalamikaji hawakuitwa.

Wakili wa Serikali Mgeni Mdee aliunga mkono rufaa hiyo akisema hati ya mashitaka inatofautiana na ushahidi uliotolewa kortini na kwamba ili kutibu hilo, upande wa mashitaka ulipaswa kuirekebisha hati ya mashitaka.

Akitoa hukumu yake, Jaji Banzi alikubaliana na hoja za mawakili hao akisema hati ya mashitaka ilionesha tukio lilitokea Novemba 19,2024 lakini mlalamikaji katika ushahidi wake anasema alivamiwa na watu hao Agosti 19,2024.

“Ni wazi kupitia ushahidi wa mlalamikaji, ni wazi kuwa tarehe ya tukio iliyotajwa katika hati ya mashitaka inatofautiana na ile iliyotajwa na mlalamikaji. Jamhuri walipaswa kuifanyia marekebisho hati ya mashitaka lakini hawakufanya,”alisema.

“Kwa hiyo mashitaka hayo hayakuthibitishwa na washitakiwa walistahili kuachiwa huru. Lakini pia kuna mkanganyiko mkubwa kati ya ushahidi wa mlalamikaji na ushahidi wa ofisa wa polisi ambaye alikagua eneo la tukio,”aliongeza Jaji.

Akitoa mfano wa mkanganyiko huo, Jaji alisema mlalamikaji alisema aliporwa Agosti 19,2024 lakini shahidi wa 4 ambaye ni polisi alidai alikagua eneo la tukio Novemba 20,2024 kukagua tukio la uporaji lililotokea Novemba 19,2024.

“Katika ukurasa wa 61 alienda mbali na kueleza kuwa Novemba 22,2024 alikamata washukiwa wa tukio lililotokea Novemba 19,2024. Kwa ushahidi huo, tukio lililotokea Agosti 19,2024 halihusiani na mlalamikaji aliyeporwa Agosti 19,2024.”

 “Kutokana na upungufu huo, huwezi kusema mashitaka dhidi ya warufani yalithibitishwa katika viwango vinavyokubalika. Kutiwa kwao hatiani hakuwezi kuegemea vielelezo vilivyopatikana kinyume cha sheria.”

Kutokana na sababu hizo, Jaji Banzi alisema Mahakama imeridhika kuwa kesi dhidi ya warufani haikuthibitishwa bila kuacha shaka, hivyo anafuta kutiwa kwao hatiani na adhabu na kuamuru waachiliwe mara moja kutoka gerezani.