BAO alilolifunga mshambuliaji wa Dodoma Jiji, Edgar William, juzi katika ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania, limemfanya kuweka raekodi ya kuwafunga maafande hao misimu miwili mfululizo, huku akiwa na timu mbili tofauti.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam, Edgar alifunga bao hilo dakika ya 50, akipokea pasi ya Salmin Hoza, likiwa ni la tatu kwake msimu huu.
Bao hilo limemfanya kuifunga JKT mara mbili kwa misimu miwili mfululizo huku akizichezea timu tofauti, akianza msimu wa 2024-2025 akiwa Fountain Gate, ambayo aliifungia moja, wakati kikosi hicho kikichapwa mabao 3-1, Mei 13, 2025.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, mshambuliaji huyo alifunga bao la Fountain dakika ya 86, baada ya JKT kufunga kupitia kwa Mohamed Bakari dakika ya sita, Shiza Kichuya dakika ya 45 na Edward Songo dakika ya 59.
Msimu huu wa 2025-2026, nyota huyo ameifunga tena JKT, ingawa safari hii akiwa na kikosi cha ‘Walima Zabibu’, likiwa ni la pili mfululizo kukifunga kikosi hicho cha maafande, tena yote kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Kabla ya kutua Dodoma Jiji, msimu wa 2024-2025, Edgar aliifungia Fountain mabao sita ya Ligi Kuu na kuasisti mawili, huku akikumbukwa msimu wa 2023-2024 alipokuwa mfungaji bora wa Championship akiwa na KenGold baada ya kufunga mabao 21.
Mbali na ufungaji bora, Edgar alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Championship msimu wa 2023-2024, akiwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye akiwa na kikosi cha KenGold na Mganda Boban Zirintusa, ambaye alikuwa Biashara United.
Nyota huyo anashikilia rekodi nzuri katika Ligi ya Championship kwani licha ya kuibuka mchezaji bora na mfungaji bora, pia amepandisha timu mbili Ligi Kuu Bara, akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha KenGold msimu wa 2023-2024.