Uchakachuaji wa tumbaku, wachelewesha bei msimu 2025/2026

Kahama. Uchafuzi wa tumbaku na kuchanganya madaraja, kumetajwa kuathiri uendelevu wa biashara ya zao hilo nchini, pamoja na kusababisha hasara kwa kampuni zinazonunua tumbaku kupitia Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (Kacu).

Hali hiyo pia imeathiri upangaji wa bei ya tumbaku kwa msimu wa 2025/26, kwenye chama hicho kikuu cha ushirika.

Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Glory Absalum, amesema hayo leo Januari 31,2026, wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 30 wa mwaka wa Kacu, na kuwataka viongozi wa vyama vya msingi kusimamia na kuhakikisha tabia hizo zinakomeshwa.

Absalum amesema migogoro mingi inayojitokeza inasababishwa na baadhi ya wakulima kutozingatia maadili, ikiwamo kuchanganya tumbaku bila kufuata madaraja husika, hali inayosababisha kushuka kwa bei na kuibua sitofahamu kati ya vyama vya ushirika na wanunuzi.

 “Niwaombe wanaushirika tuwe waaminifu, tusichanganye madaraja, soko linashuka, tunakuwa na migogoro mara kwa mara kwenye vyama, tunaomba tufunge tumbaku kulingana na maelekezo ya madaraja,” amesema Absalum.

“Vyama vya msingi vimeanzishwa ili vitusaidie, tusifanye sehemu ya sisi kujificha kufanya vitu ambavyo haviko kiutaratibu. Viongozi wa vyama vya ushirika hakikisheni mnasimamia taratibu na kanuni ili vyama vya msingi viweze kuwa imara kwa maendeleo ya ushirika.”

Mwenyekiti wa Kacu, Emanuel Nyambi amekiri kuwepo kwa changamoto ya uchafuzi wa tumbaku hali inayotishia kuporomoka kwa bei ya zao hilo.

“Ni kweli changamoto hiyo ipo, tumejipanga kufanya usimamizi na wanachama na wakulima wanaona kabisa mpaka leo bei za madaraja bado hazijatoka na changamoto kubwa ni hii ya ufichiaji wa vitu visivyokuwa tumbaku,” amesema Nyambi

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Shinyanga, Ibrahim Kakozi amesema mkulima atakayekugundulika kuchafua tumbaku atashtakiwa kama kesi ya jinai na ofisi yake haitamvumilia yeyote atakayekutwa na kosa hilo.

“Kila mmoja asimame kwenye nafasi yake, tuache siasa kama tunataka kukomesha hali hii, mimi sitakubali, hii ni jinai tusijadili jadili tukibaini mtu yeye mwenyewe ahusike.”

Katika msimu wa kilimo 2025/26 Kacu imeingia mkataba na kampuni 12 kwa ajili ya kuzalisha na kuwauzia jumla ya kilo milioni 20.05 za tumbaku, zikiwamo kilo milioni 19.68 za tumbaku ya mvuke (Fcv) na kilo 375,000 za tumbaku ya hewa (Burley).

Kutokana na hali halisi ya upandaji wa tumbaku ya mvuke hadi kufikia Desemba 31,2025, jumla ya hekta 20,015 sawa na asilimia 85.47 ya lengo la hekta 13,057 za mkataba zilikuwa zimeshapandwa na zinatarajia kuzalisha jumla ya kilo milioni 16.82.

Hata hivyo, hadi kufikia Desemba 31, 2025 hakuna maafikiano yaliyofikiwa kuhusiana na bei ya tumbaku kwa msimu huu.