Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2025, yakionesha picha mseto ya ufaulu ambapo wasichana wameongoza kwa idadi ya waliofaulu, huku wavulana wakionesha ubora wa juu zaidi wa ufaulu kwa madaraja ya juu.
Matokeo hayo yanaonesha kuwa ufaulu umeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2024, hali inayoashiria maendeleo katika sekta ya elimu licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika baadhi ya masomo, hususan sayansi na hisabati.
Akizungumza leo Januari 31, 2026 wakati wa kutangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Necta, Profesa Said Mohamed amesema jumla ya watahiniwa 526,620 sawa na asilimia 94.98 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne.
Ufaulu huo ni ongezeko la asilimia 2.61 ikilinganishwa na matokeo ya mtihani wa mwaka 2024 uliokuwa asilimia 92.37.
Kwa mujibu wa Profesa Mohamed, wasichana walikuwa wengi zaidi miongoni mwa watahiniwa waliofanya mtihani huo.
Jumla ya wasichana 295,032 walifanya mtihani wa kidato cha nne, ambapo 278,108 sawa na asilimia 94.26 walifaulu.
Kwa upande wa wavulana, watahiniwa 259,426 walifanya mtihani huo na kati yao 248,512 sawa na asilimia 95.79 walifaulu.
“Tofauti iliyopo ni kwamba ubora wa ufaulu wa madaraja ya kwanza hadi ya tatu umeonekana kuwa mzuri zaidi kwa wavulana, wakati wasichana wakiwa wengi zaidi kwa idadi ya wanaofaulu,” amesema Profesa Mohamed.
Akizungumzia hilo mchambuzi wa elimu, Stella Mrema amesema takwimu hizo zinaonesha tofauti ya kimfumo katika namna wanafunzi wa kike na wa kiume wanavyojiandaa na kushindana kielimu.
“Wasichana wamekuwa na nidhamu nzuri ya kuhudhuria masomo na kumaliza shule, ndiyo maana wanaongoza kwa idadi ya wanaofaulu. Hata hivyo, wavulana wanaonekana kuwekeza zaidi kwenye masomo yanayowapa alama za juu, jambo linalowaweka juu katika ubora wa ufaulu,” amesema.
Mtaalamu wa mitalaa, Anna Kweka, amesema ufaulu wa asilimia karibu 95 ni mzuri kitaifa, lakini maswali makubwa yako kwenye masomo ya sayansi
Profesa Mohamed amesema katika somo la fizikia, ufaulu umeongezeka kutoka asilimia 32.59 mwaka 2024 hadi asilimia 44.21 mwaka 2025, huku hisabati ikiendelea kuwa na ufaulu wa chini, ambapo ni asilimia 26.45 pekee ya watahiniwa waliofaulu.
Biolojia nalo limeonesha kushuka kwa ubora wa ufaulu kwa asilimia 15.12, huku waliofaulu wakiwa asilimia 65.68.
“Haya ni masomo yanayounda msingi wa sayansi na teknolojia. Kama bado tuna wanafunzi zaidi ya asilimia 70 wanaofeli hisabati, lazima tukubali kuwa tatizo ni la kimfumo,” amesema Kweka.
Kwa upande wa masomo ya lugha, wachambuzi wanasema matokeo yanatia moyo. Takwimu zinaonesha asilimia 97.82 ya watahiniwa wamefaulu Kiswahili, huku Kiingereza, Kifaransa na Kichina yakifanya vizuri kwa ufaulu wa kati ya asilimia 79.48 hadi 93.43.
Hata hivyo, somo la Kiarabu limeendelea kuwa na ufaulu wa chini licha ya kuongezeka hadi asilimia 50.62 kutoka asilimia 33.86 mwaka 2024.
Masomo ya sayansi ya jamii nayo yameonesha ongezeko la ufaulu, ambapo jiografia imeongoza kwa kupanda kwa asilimia 7.55, ikifuatiwa na historia kwa asilimia 4.87.
Mchambuzi wa elimu ya jamii, Rehema Kiwelu, amesema masomo haya yanafaulu kwa sababu yanahusiana zaidi na maisha ya kila siku ya mwanafunzi.
“Masomo yanayohusisha mifano halisi na mjadala huongeza uelewa. Hili ni funzo kwa masomo ya sayansi,” amesema.
Katika hatua nyingine Necta imefuta matokeo ya watahiniwa 77 waliobainika kufanya udanganyifu, wakiwamo 30 wa shule na 47 wa kujitegemea.
Aidha, matokeo ya watahiniwa wawili yamefutwa baada ya kuandika lugha ya matusi kwenye karatasi za majibu.
Akizungumzia kuendelea kujitokeza kwa vitendo vya kuandika matusi kwenye karatasi za majibu, Profesa Mohamed amesema Necta imefanya utafiti kubaini chanzo cha tatizo hilo na kwa sasa ipo katika hatua ya kuchambua matokeo ya utafiti huo.
“Suala la kuandika matusi ni la kimaadili zaidi. Tumefanya utafiti na tunaendelea kuchambua tulichokibaini. Tutakapokamilisha uchambuzi huo, tutaweka wazi taarifa. Kwa upande wetu wa kitaaluma, msisitizo ni kuhakikisha ujifunzaji na ufundishaji vinafanyika ipasavyo, lakini pia tunawaomba wanajamii kushiriki kuzungumzia suala la maadili,” amesema.