Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikijitenga na sakata la tuhuma za wizi wa fedha za mchango kwa ajili ya mwenyekiti wake, Tundu Lissu, chanzo cha habari kimeidokeza Mwananchi namna fedha hizo zilivyogawanywa miongoni mwa makada.
Jana, Januari 29, 2026, familia ya mwanasiasa huyo ilieleza kuwa viongozi wa juu wa Chadema wasihusishwe katika sakata hilo, bali ni makada wachache wa chama hicho ndiyo waliokwenda kinyume na makubaliano.
Januari 28, 2026, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo alitoa taarifa kwa umma, akitangaza jeshi hilo kumshikilia Fredrick Mbwambo kwa tuhuma za wizi wa fedha zilizochangwa kwa ajili ya kumsaidia Lissu.
Taarifa ya Kamanda Masejo inaeleza kuwa, Mbwambo alikamatwa Januari 27, 2026 mkoani humo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa kaka yake Lissu, Alute Mughwai aliyebaini wizi wa fedha hizo zilizokuwa zimechangwa kwa ajili ya Lissu.
Alipotafutwa kuzungumzia mwenendo wa sakata hilo, leo Januari 30, 2026, Kamanda Masejo amesema bado wanaendelea kufuatilia suala hilo.
Ingawa katika taarifa ya polisi haikubainishwa kiwango cha wizi uliotokea, taarifa ambazo Mwananchi linazo zinadai kuwa, kati ya Sh41 milioni zilizochangwa, Sh22 milioni ndizo zilikabidhiwa kwa familia ya Lissu huku Sh19 milioni hazikujulikana zilipo.
Vincent Mughwai, mdogo wake Lissu, aliiambia Mwananchi, jana kuwa, harambee ya kumchangia Lissu ilifanywa na vijana na marafiki wa Chadema kwa ajili ya kumsaidia mwenyekiti huyo, ikiongozwa na Mbwambo (anayeshikiliwa na polisi).
Chanzo cha kuaminika kimeeleza kuwa, mchakato wa kampeni ya kuhamasisha mchango wa Lissu uliopewa jina la ‘Funga Mwaka na Tundu Lissu’ uliendeshwa na Mbwambo na makada wengine wa Chadema, majina yamehifadhiwa (wanaishi nchi jirani).
Taarifa zinadai kuwa, makada walifanya kampeni ya uhamasisha kupitia makundi ya mitandao ya kijamii katika wiki ya mwisho wa Desemba 2025.
Chanzo hicho kinadai kuwa, usiku wa Desemba 31, 2025 ndio ilikuwa siku ya mwisho wa kuchangisha na tangazo likawekwa kuwa zimepatikana Sh26 milioni, lakini uhalisia ilikuwa Sh41 milioni.
Baada ya hapo, Mughwai alikabidhiwa Sh22 milioni na inasemekana alipata wasiwasi na kwenda kujiridhisha kupitia taarifa za miamala na kubaini kiwango kilichopatikana ni zaidi ya alichokabidhiwa.
Pazia la mchango huo lilipofungwa, inadaiwa Sh6 milioni zilitumwa kwenda nchi jirani (Nairobi -Kenya) kupitia namba ya wakala wakati Sh2 milioni zikitumwa kupitia namba ya mkononi ya mtandao mmoja wa Tanzania.
Juzi, katika taarifa yake, Kamanda Masejo alisema: “Ufuatiliaji wa awali umeonesha kuwa, ukusanyaji huo wa fedha ulikuwa ukifanywa kupitia namba mbili za simu za kampuni tofauti, inadaiwa zilihamishiwa kwenye namba mbili za simu, moja ikiwa ni ya kampuni ya Tanzania na ya pili ni kampuni ya simu ya nchi jirani.”
Inadaiwa kuwa, Sh700,000 zilitumwa katika namna hiyo hiyo iliyopokea awali Sh2 milioni, lakini baada ya jambo hilo kufika Jeshi la Polisi, liliamua Sh 2milioni zilirudishwe kwenye akaunti ya Mughwai.
Aidha, inadaiwa Sh3 milioni zilitumwa kwenye namba nyingine ya Kitanzania. Hiyo ni baadhi ya miamala mikubwa iliyofanywa katika mgawanyo wa fedha za mchango wa Lissu ikichepushwa kutoka kwenye namba maalumu zilizosajiliwa kwa jina la Mughwai.
Wakati huohuo, uongozi wa Chadema ulitoa ufafanuzi kuwa, mchango wa Lissu uliratibiwa kupitia namba ya simu ya kaka yake (Mughwai) na upokeaji wa michango haukufanywa na sekretarieti ya Taifa au kiongozi yeyote wa chama hicho.
“Kumekuwepo na taarifa za upotoshwaji zinazosambazwa na watu wasiokitakia mema (Chadema) zikiwahusisha viongozi wa chama na kashfa zinazohusisha madai ya michango iliyoendeshwa hivi karibuni mtandaoni kumchangia Lissu.
“Tunawaomba Watanzania na dunia nzima kupuuza taarifa potofu zinazosambazwa kwa lengo la kuchafua taswira ya chama na viongozi wake,” alieleza Brenda Rupia ambaye ni Mkurungenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa Januari 29, 2026.
Kwa mujibu wa Rupia, Chadema ni taasisi inayoongozwa kwa misingi ya uadilifu, uwazi na maadili, hairuhusu matumizi ya jina la chama au viongozi wake kufanikisha vitendo vinavyokiuka sheria na taratibu zilizopo.