Utitiri wa ving’ora barabarani: Serikali yatangaza hatua kali

Dar es Salaam. Serikali imetangaza kuanza kampeni maalumu ya kudhibiti matumizi holela ya ving’ora barabarani pamoja na matumizi ya namba za usajili wa magari zisizotambuliwa kisheria, hatua inayolenga kurejesha nidhamu, usalama na heshima kwa vyombo vya dharura.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, wakati wa ziara yake ya kwanza katika Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji tangu ateuliwe kuongoza wizara hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan. Katika ziara hiyo, aliyoambatana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Ayoub Mohamed Mahmoud.

Hatua hiyo imetangazwa na Serikali ikiwa siku chache zimepita tangu gazeti la Mwananchi kuandika habari iliyoshapishwa Januari 28, 2026 iliyokuwa na kichwa ” Hofu yatanda magari yenye chesisi namba” ikielezea yanavyotumika hadi usiku wa manane bila usajili wananchi, wakiyataja kuhusika na matukio ya uhalifu.

Akizungumza katika ziara hiyo, Leo Jumamosi, Januari 31,2026 Waziri Katambi amesema matumizi yasiyodhibitiwa ya ving’ora, hususan katika magari ya watu binafsi yasiyotambuliwa na Kanuni za Usalama Barabarani, yamekuwa kikwazo kikubwa kwa vyombo vya dharura kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Magari ya zimamoto huwashwa king’ora ili kupisha na kutoa huduma za dharura, lakini madereva wengi hawazingatii kwa sababu ya kuzoea kelele za ving’ora visivyokuwa halali. Kitendo hiki ni hatari na kinahatarisha maisha ya wananchi,” amesema Katambi.

Amesema serikali iko katika hatua za mwisho za kuchukua hatua kali dhidi ya matumizi hayo, akieleza kuwa hali ya sasa imegeuka kuwa vurugu kutokana na kila mtu kufunga king’ora bila ruhusa.

 “Ninawasihi wananchi kuheshimu ving’ora vya magari ya wagonjwa, zimamoto na misafara ya viongozi. Serikali sasa inaelekea kuondoa ving’ora vyote visivyotambuliwa kisheria,” amesema.

Waziri Katambi amesema changamoto ya ujenzi holela na kutokuzingatia kanuni za usalama wa moto imekuwa ikirudisha nyuma jitihada za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kutoa huduma za haraka pale majanga yanapotokea.

 “Baadhi ya watu hujenga katika njia za kupita magari ya zimamoto au hukwepa ukaguzi wa vifaa vya kuzima moto kwa kigezo cha gharama, ilhali gharama kubwa zaidi ni kupoteza maisha na mali,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema serikali nalitambua na kulithamini Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa mchango wake mkubwa katika kuokoa maisha na mali za Watanzania, na akaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu ili kuimarisha ufanisi wake.

Naye Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga, amesema kuwa kwa mwaka 2025 jumla ya matukio ya moto 3,091 yaliripotiwa nchini, ambapo watu 114 walipoteza maisha huku 295 wakijeruhiwa.