Uwanja wa Afcon wafikia asilimia 30 Zanzibar

Unguja. Wakati maandalizi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 yakiendelea, ujenzi wa uwanja utakaotumika katika michuano hiyo umefikia asimilia 30 Zanzibar.

Uwanja huo unaojengwa Fumba Mkoa wa Mjini Magharibi na kampuni ya Orkun ya Uturuki, umeanza kujengwa Mei 2025 na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu kwa awamu ya kwanza kwa gharama ya Dola za Marekani 150 milioni (Sh389.141 bilioni).

Akizungumza baada ya kufanya ziara maalumu ya kukagua na  kutembelea uwanja huo leo Januari 31, 2026, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali inaridhishwa na hatua zilizofikiwa za mradi huo.

Ujenzi wa uwanja utakaotumika katika michuano ya Afcon 2027 ukiwa unaendelea Fumba Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Zanzibar.



“Tumeona hali halisi ya maendeleo ya ujenzi, kazi inaendelea vizuri, na kwa hakika uwanja huu wapo pazuri katika hatua zake za ujenzi na wapo ndani ya muda.

“Nataka niwahakikishie wananchi kwamba kazi hii itaendelea vizuri kwasababu vifaa vyote vinavyohitajika vipo tayari kwenye eneo la ujenzi, kwahiyo hakuna sababu ya kazi hii kuchelewa,” amesema Hemed

Amesema azima ya serikali ipo palepale kutumia uwanja huo kwa michezo ya AFCON 2027.

Amesema kwamba viongozi wa Shirikisho la Mpira Afrika (CAF) walitembelea uwanja huo jana na wameridhika na kiwango ambacho kimefikiwa cha ujenzi wake.

Katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watu 36,500, kutakuwa na eneo la kuegesha magari zaidi ya 2000 kwa wakati mmoja.

Awamu ya kwanza ya ujenzi huo, inahusisha uwanja na barabara za ndani na maegesho  huku awamu ya pili itahusisha ujenzi wa hoteli ya nyota tano, hospitali ya michezo na viwanja vya michezo.

Ujenzi wa uwanja utakaotumika katika michuano ya Afcon 2027 ukiwa unaendelea Fumba Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Zanzibar.



Amesema baada ya uwanja kukamilika wataona ni fursa zipi za kibiashara zinazopatikana katika maeneo haya.

“Niwaombe wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wanaotaka kuja kuwekeza huku. Tujiandae basi kutakuwa kuna mji wa biashara kabisa, kwa hiyo kutakuwa na soko la vitu vingi kwa hiyo ni fursa kwa wawekezaji kuja kuwekeza,” amesema

Naye Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Riziki Pembe Juma amesema wizara inaendelea kusimamia hatua hizo ili lengo lililokusudiwa lifikiwe.

“Huu mradi baada ya kukamilika, Zanzibar itajiwa na ugeni mkubwa ambao utatoa fursa kwa watu wengi na kupata neema kubwa,” amesema.

Kwa mujibu wa Pembe, muda utakapofika wataandaa utaratibu mzuri wa wajasiriamali kwenda kuonesha na kuuza bidhaa zao katika eneo hilo ili waweze kunufaika na ujio wa mashindano hayo katika eneo la nyumbani.

“Hii ni fursa ya wote, wakae mkao wa kula, kikubwa tuendelee kuimarisha biashara zetu ili wakati ukifika tupate kunufaika.

“Mbali na wajasiriamali wadogo lakini ujio wa mashindano hayo watafaidika watu wa hoteli, wenye magari ya usafiri, kwa hiyo zitakuwa fursa kubwa kwa wananchi wetu,” amesema Pembe.

Amesema licha ya kuwapo na kamati kuu ya kitaifa, inayoratibu masuala ya AFCON, lakini Zanzibar yenyewe inaendelea kufuatilia kwa ukaribu kazi na mipango yote kwa ajili ya fainali hizo.

Kwa upande wake Abdulhamid Mhoma mmiliki wa kampuni ya Al-Hatmy Design and Engineering Consultancy inayosimamia mradi huo, amesema wanaendelea vizuri na wanaamini watamaliza kwa wakati.

“Kwa mujibu wa programu yetu, tumeshafikia asilimia 30 kati ya 100 na hivi mnavyoona tumeshaweka ngazi ya kwanza ya zege baadaye itakuja ya pili na ya tatu kisha ndio itakuja paa ambalo kwa sasa linatengenezwa Uturuki italetwa hapa kwa meli,” amesema

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, wamekusudia baada ya miezi mitatu wamalize kazi zote za kumwaga zege.

“Kwa hiyo Desemba kiwanja kitakuwa kimeshamalizika na itakuwa imebaki kazi kidogo za mapambotu,” amesema Mhoma.