Wafanyabiashara Soko la Nguzo walia na tozo, miundombinu chakavu

Shinyanga. Wafanyabiashara wa Soko la Nguzo Nane lililopo Manispaa ya Shinyanga, mkoani Shinyanga, wamezungumzia kero na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo katika shughuli zao za kila siku, hali wanayosema inakwamisha ufanisi wa biashara ndani ya soko hilo.

Wakizungumza leo Jumamosi Januari 31, 2026 wakati wa ziara ya kushtukiza iliyofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita wafanyabiashara hao wamesema changamoto kubwa zinazowakabili ni miundombinu mibovu ya maji taka, uchakavu wa vibanda, mitaro isiyopitisha maji ipasavyo pamoja na ushuru unaodaiwa kuwa mkubwa.

Mfanyabiashara wa soko hilo, Amina Said amesema, mitaro inayopitisha  ya mvua sokoni hapo imeziba hali inayosababisha eneo hilo kushindwa kupitika wakati wa mvua, sambamba na vibanda kuwa chakavu.
“Mitaro ya soko hili haipitishi maji, mvua ikinyesha hapa hapapitiki. lakini vibanda navyo vimechakaa sana. Tunaomba tujengewe soko kwa sababu hali si nzuri,” amesema Amina.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa chakula Jenifa Mbunda, amesema ushuru wa taka ni mkubwa kwa wafanyabiashara wa chakula ukilinganisha na kiwango cha uchafu wanaozalisha.
“Sisi mamantilie tunazalisha uchafu mdogo kwa siku ukilinganisha na wauzaji wa mbogamboga, lakini tunatozwa Sh5,000 wakati wao (wa mbogamboga) wanalipa Sh2,000. Tunaomba tupunguziwe ushuru kwa sababu gharama ni kubwa na wakati mwingine chakula tunakilaza kwa kukosa wateja,” amesema Jenifa.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Biashara wa Manispaa ya Shinyanga, Shamim Shaban amesema uongozi wa manispaa unaendelea kuboresha miundombinu ya masoko kwa awamu.
“Awamu ya kwanza tulianza katika Soko Kuu la Manispaa pamoja na masoko mengine, na tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya kufanya ukarabati na uboreshaji wa Soko la Nguzo Nane,” amesema Shamim.

Kufuatia malalamiko hayo, Mhita ametoa maagizo kwa uongozi wa Manispaa ya Shinyanga kuhakikisha ndani ya miezi mitatu ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya soko hilo uwe umeanza kutekelezwa.
“Soko hili linahudumia asilimia kubwa ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga. Kwa kuwa fedha tayari zimetengwa katika robo hii ya mwaka, ukarabati wa soko hili lazima uwe umeanza, na nitapita kukagua utekelezaji wake,” amesema Mhita.