Yanga, Al Ahly CAFCL hakuna mbabe

YANGA SC imelazimishwa sare nyumbani ikimaliza dakika 90 ikifungana bao 1-1 dhidi ya Al Ahly katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kundi B iliyochezwa leo Januari 31, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Sare hiyo inaifanya Yanga kufikisha pointi tano wakati Al Ahly ikiongeza alama moja na kuwa nane huku Waarabu hao wakiendelea kuongoza kundi B la michuano hiyo.

Yanga haikunza kwa kasi sana, dakika 45 za kwanza ilikuwa taratibu huku ikipoteza mipira wakati inajenga mashambulizi yake.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alikuwa na wakati mgumu kipindi cha kwanza, akionekana akiongea kwa ukali wakati alipoona wachezaji wake wanafanya makosa.

Dakika ya 10, Yanga ilitengeneza nafasi nzuri, winga wake Allan Okello alipiga shuti kali lakini likapanguliwa na kipa Mostafa Shoubir na kurudi uwanjani, kisha kumkuta Chadrack Boka akamuwekea pasi nzuri Laurindo Aurelio ‘Depu’, hata hivyo shuti lake likapaa.


Nafasi nyingine nzuri kwa Yanga ilipatikana dakika ya 30, Pacome Zouzoua aliwapangua mabeki wa Al Ahly na kukutana na kipa Shoubir lakini shuti lake likapanguliwa na mlinda mlango huyo na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuwa na madhara.

Al Ahly ilitengeneza nafasi nzuri dakika ya 42, Ahmed Sayed ‘Zizou’ alifika vizuri eneo la hatari lakini pasi yake ya mwisho ikimtafuta nahodha wake Mahmoud Ibrahim ‘Trezeguet’ ikanaswa na mabeki wa Yanga.

Yanga ikapata bao dakika ya 45 likitengenezwa kwa pasi za haraka ikimuhisha Okello kisha Depu na Pacome, mpira uliokuwa unaokolewa na beki wa Al Ahly ukamkuta Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na kumalizia kirahisi bao ambalo likaifanya Yanga kwenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0 .

Kipindi cha pili, Al Ahly ilirudi na nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 59, mfungaji akiwa Aliou Dieng akimalizia kwa shuti mpira aliounasa wakati Yanga ikipambana kuzima shambulizi la kona.

Baada ya sare hiyo, Yanga sasa inakwenda Morocco kucheza dhidi ya AS FAR Rabat, mechi inayotarajiwa kuchezwa Februari 7, 2026, kisha itamalizia nyumbani hatua ya makundi Februari 13, 2026 ikiikaribisha JS Kabylie.