Yanga ilivyoisimamisha Al Ahly ikipiga hesabu kali kufuzu robo fainali

SI umeona Yanga ilivyotoana jasho na Al Ahly, timu yenye historia kubwa katika soka la Afrika ikibeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara 12 na kuwa kinara? Sasa Wanajangwani hao vichwani mwao wanapiga hesabu kali za kumalizana na Waarabu wengine wawili.

Yanga baada ya kumalizana na Al Ahly, sasa inaingia kwenye hatua nyingine ambapo mechi mbili zijazo italazimika kuzicheza kwa hesabu kubwa ili kuvuka hatua ya makundi na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hiyo inatokana na kundi B linavyoonekana kwa sasa baada ya leo Januari 31, 2026 kulazimishwa sare nyumbani ikimaliza dakika 90 kwa kufungana bao 1-1 na Al Ahly kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Sare hiyo inaifanya Yanga kufikisha pointi tano wakati Al Ahly ikiongeza alama moja na kuwa nane, huku Waarabu hao wakiendelea kuongoza kundi hilo la michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika.

Hata hivyo, kundi hilo linasubiri mechi ya baadaye usiku kati ya AS FAR Rabat na JS Kabylie, timu zenye pointi mbili ili kuona Yanga hesabu zake ipige kwa namna gani iweze kufuzu robo fainali kibabe.

Yanga haikunza kwa kasi sana dakika 45 za kwanza mbele ya Al Ahly, ilikuwa taratibu huku ikipoteza mipira wakati inajenga mashambulizi.

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alikuwa na wakati mgumu kipindi hicho akionekana kuzungumza kwa ukali wakati alipoona wachezaji wake wanafanya makosa.

Katika dakika ya 10 Yanga ilitengeneza nafasi nzuri ambapo winga wa kulia Allan Okello alipiga shuti kali langoni kwa wapinzani wao, lakini lilipanguliwa na kipa Mostafa Shoubir na kurudi uwanjani kisha kumkuta Chadrack Boka akamuwekea pasi nzuri Laurindo Aurelio ‘Depu’, hata hivyo shuti lake lilipaa juu.


Nafasi nyingine nzuri kwa Yanga ilipatikana dakika ya 30 pale Pacome Zouzoua alipowapangua mabeki wa Al Ahly na kukutana na kipa Mostafa Shobeir, lakini shuti lake lilipanguliwa na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuwa na madhara.

Al Ahly ilitengeneza nafasi nzuri dakika ya 42, Ahmed Sayed ‘Zizou’ akifika vizuri eneo la hatari, lakini pasi yake ya mwisho ilimtafuta nahodha wake Mahmoud Ibrahim ‘Trezeguet’ ikanaswa na mabeki wa Yanga.

Mabingwa wa Ligi Kuu Bara walipata bao dakika ya 45 likitengenezwa kwa pasi za haraka iliyomhusha Okello kisha Depu na Pacome, mpira uliokuwa unaokolewa na beki wa Al Ahly ukamkuta Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na kumalizia kirahisi bao ambalo liliifanya Yanga kwenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0 .

Kipindi cha pili, Al Ahly ilirudi na nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 59 mfungaji akiwa Aliou Dieng akimalizia kwa shuti mpira aliounasa wakati Yanga ikipambana kuzima shambulizi la kona.

Baada ya sare hiyo, Yanga sasa inakwenda Morocco kucheza dhidi ya AS FAR Rabat, mechi inayotarajiwa kuchezwa Februari 7, 2026, kisha itamalizia nyumbani hatua ya makundi Februari 13, 2026 ikiikaribisha JS Kabylie.

Baada ya mchezo kumalizika mashabiki wa Yanga waliokuwapo uwanjani walionyesha kufurahishwa na matokeo, huku wakiwa na matumaini kwamba timu yao itafanikiwa kufuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo kupitia mechi mbili zilizobaki.

Yanga: Djigui Diarrra, Dickson Job, Ibrahim Abdullah, Bakari Mwamnyeto, Chadrack Boka/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Mohammed Camara, Duke Abuya, Maxi Nzengeli, Allan Okello/Israel Mwenda, Pacome Zouzoua, Laurindo Aurelio ‘Depu’/Prince Dube.

Al Ahly: Mostafa Shoubir, Mohammed Hany, Ahmed Abdelaal, Yasser Ibrahim, Yassin Mostafa, Marawan Atia, Ahmed Sayed’Zizou’, Aliou Dieng, Taher Mohammed, Mahmoud Ibrahim ‘Trezeguet’, Marwan Mohammed.