Askari Wapya Jwtz Wahitimu Mafunzo

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amefunga rasmi Mafunzo ya Askari wapya katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi (RTS) Kihangaiko Msata Mkoani Pwani leo tarehe 31 Januari 2025.

Jenerali Mkunda amewataka askari wapya kukiishi na kuzingatia kiapo cha utii wakati wote watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao sehemu mbalimbali watakayopangiwa, huku akisisitiza kuchukuliwa hatua kwa askari watakaokwenda kinyume na kiapo chao.

Askari wapya wameaswa kutotenda mambo ambayo ni kinyume na taratibu za kijeshi ikiwemo kutojihusisha na siasa, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, matumizi ya madawa ya kulevya, michezo ya kamari na kuepuka madeni yasiyo na tija.

Mkuu wa Majeshi amewataka Askari hao kutunza Afya zao na kuzingatia lishe bora wakati wote wanapotekeleza majukumu yao. Aidha, wasijihusisha na uhalifu wa aina yoyote kwani watakuwa wamekwenda kinyume na sheria na taratibu za kijeshi hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Jenerali Mkunda amesisitiza Askari hao kuwa tayari kiakili na kisaikolojia kuitetea nchi kwa kutekeleza majukumu ya Jeshi ndani na nje ya Tanzania.

Naye, Mkuu wa Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi Kihangaiko Brigedia Jenerali Sijaona Michael Myala ametoa pongezi kwa Askari wapya waliohitimu mafunzo na kuwa tayari kukabiliana na changamoto za kiusalama.

Brigedia Jenerali Myala amesema Askari wapya wapo tayari kutekeleza majukumu mbalimbali ya kijeshi kutokana na mafunzo waliyoyapata. Shule ya RTS Kihangaiko itaendelea kushirikiana na Makao Makuu ya Jeshi kuboresha mazingira ya Mafunzo ili kuendelea kuwafunza vijana kuwa askari Hodari watakaokuwa na uwezo wa kushiriki katika ulinzi ndani na nje ya nchi.

Askari wapya Kundi la 44/25 waliohitimu mafunzo wapo tayari kushiriki katika majukumu ya ulinzi wa taifa hasa katika mipaka ya nchi na kutambua majukumu yao mengine yakiwemo kumtii na kumlinda Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu na kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.