Msata, Pwani. Askari wapya wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliohitimu mafunzo Msata mkoani Pwani, wametakiwa kukiishi kiapo cha utii wakati wote watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao katika sehemu mbalimbali watakazopangiwa.
Katika hilo, wameaswa kutotenda mambo ambayo ni kinyume na taratibu za kijeshi, ikiwemo kutojihusisha na siasa, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, matumizi ya dawa za kulevya, michezo ya kamari na kuepuka madeni yasiyo na tija.
Akizungumza wakati akifunga rasmi mafunzo ya askari hao wapya katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi (RTS) Kihangaiko, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, amesema askari watakaokwenda kinyume na kiapo chao watachukuliwa hatua.
Askari wapya wa JWTZ wakila kiapo katika mahafali yaliyofanyika Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi (RTS), Kihangaiko, Msata mkoani Pwani mara baada ya kumaliza mafunzo.
Amewataka askari hao kutunza afya zao na kuzingatia lishe bora wakati wote wanapotekeleza majukumu yao.
Aidha, amewasisitiza wasijihusishe na uhalifu wa aina yoyote, kwani watakuwa wamekwenda kinyume na sheria na taratibu za kijeshi, hivyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Jenerali Mkunda amesisitiza askari hao kuwa tayari kiakili na kisaikolojia kuitetea nchi kwa kutekeleza majukumu ya Jeshi ndani na nje ya Tanzania.
Askari wapya wa JWTZ wakila kiapo katika mahafali yaliyofanyika Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi (RTS), Kihangaiko, Msata mkoani Pwani mara baada ya kumaliza mafunzo.
Naye, Mkuu wa Shule ya Mafunzo ya Awali ya Kijeshi Kihangaiko, Brigedia Jenerali Sijaona Myala, amewapongeza askari hao waliohitimu mafunzo na kuwa tayari kukabiliana na changamoto za kiusalama.
Brigedia Jenerali Myala amesema askari wapya wapo tayari kutekeleza majukumu mbalimbali ya kijeshi kutokana na mafunzo waliyoyapata.
“Shule ya RTS Kihangaiko itaendelea kushirikiana na makao makuu ya jeshi kuboresha mazingira ya mafunzo ili kuendelea kuwafunza vijana kuwa askari hodari watakaokuwa na uwezo wa kushiriki katika ulinzi ndani na nje ya nchi,” amesema.